Friday, August 25, 2023

TUWASAIDIE WAWEKEZAJI WA BIDHAA ZA AFYA BADALA YA KUWA VIKWAZO: DKT. MOLLEL.

 

Na Rayson Mwaisemba WAF - DSM.

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa mamlaka na taasisi zinazosimamia bidhaa za afya ikiwemo Dawa, vifaa tiba pamoja na vitendanishi kuwasaidia Wafanyabiashara wa bidhaa hizo kufanya biashara kwa mujibu wa Sheria na taratibu badala ya kuwa vikwazo ili wananchi wanufaike na bidhaa hizo kwa gharama nafuu na kwa ubora unaotakiwa.

Dkt. Mollel ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam, alipofungua Mkutano wa Wawekezaji wa bidhaa za dawa na Wafamasia, wenye lengo la kuwakutanisha Wafanyabiashara hao ili kujadili changamoto zao na mbinu mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa bidha za dawa zenye ubora na kwa gharama nafuu kwa wanachi.

"Najua wapo baadhi ya Wataalamu wetu hawana jicho la kibiashara, wengi wanaambiwa Wasaidie watu kufanya biashara wao wanageuka polisi badala ya kuwa wasaidizi ili kuwasaidia wafanyabiashara, wengi wanakaa ofisini tu badala ya kumsaidia mfanyabiashara aanzishe biashara yeye anaangalia kasoro tu." Amesema Dkt. Mollel

Amesema, Serikali ya Rais Dkt. Samia itaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili Watanzania wenye hali zote wanufaike na huduma za dawa na vifaa tiba kwa ubora na gharama nafuu, kwani wawekezaji wanasaidia Serikali kuboresha huduma hizo hasa kipindi Watanzania wanapohitaji huduma hizo kwa haraka.

Kwa upande wake Rais wa Chama the Wafamasia Tanzania Bw. Fadhili Hezekia amesema maonesho haya ya pili ya Wafamasia ni maonesho mahususi ya huduma za afya kwa Sekta nzima yanayotoa fursa kwa Watanzania kupata huduma mbalimbali za afya katika maonesho hayo.

Ameendelea kusema, maonesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwatafuta na kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani ili kuanzisha viwanda vya bidhaa za dawa nchini hali itayosaidia kupunguza gharama za dawa na kuongeza upatikanaji wake kwa ubora ule ule.

Vile vile amewataka Watanzania hasa walio katika kada ya Ufamasia kuja katika viwanja vya Diamond Jubilee ili kujifunza na kubadilishana uzoefu na Wataalamu wengine kutoka nchi mbalimbali utaosaidia kuongeza ufanisi katika eneo la dawa kwa Wataalamu wa ndani.

Sambamba na hilo, amemwomba Naibu Waziri kusaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo ikiwemo kutoa elimu kwa mamlaka nyingine ili Wafanyabiashara wanaokuja kuwekeza nchini wasipate changamoto yoyote itayopelekea kukata tamaa kuja kuwekeza katika nchi ya Tanzania.







No comments:

Post a Comment