Wednesday, August 23, 2023

POLISI BAGAMOYO WATAKIWA KUBADILIKA KIUTENDAJI.


 Askari Polisi Wilaya ya Bagamoyo wametakiwa Kubadilika kifikra na kufanya kazi kwa weledi na kuachana na utendaji kazi wa mazoea.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, (ACP) Pius Lutumo  wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa kuangalia utendaji wa kazi Wilayani hapo  wakati akizungumza na Maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ambapo amewataka kuzingatia ufanyaji kazi kwa mujibu wa Sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kupeleka utendaji usioridhisha.


Pia, Kamanda Lutumo amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi kwa kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili vitakavyolichafua Jeshi ambavyo huweza kusababisha kufukuzwa kazi.


Kadhalika, amewataka askari kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya utendaji bora kwa kutenda haki kwa tunao wahudumia vituoni " Wananchi hawapendi kuja kwenye vituo vyetu ila wanafika kwa kuwa wanashida zinazohitaji kusaidiwa nasi hivyo ni jukumu letu kuwapa huduma bora wanapofika kwenye vituo vyetu vya Polisi”, Alisema.


Aidha, amewakumbusha askari umuhimu wa kutunza vizuri vielelezo na kutokuwa na tamaa au kushawishika katika kuiba vielelezo hivyo viwapo kituoni. "Ni jukumu letu kulinda vielelezo vilivyopo kituoni na kuhakikisha vinatunzwa vizuri na siyo kuwa sehemu ya upotevu wa vielelezo hivyo ambavyo vitatumika kama ushahidi Mahakamani.


Kutoka Dawati la Habari
Polisi (M) Pwani.



No comments:

Post a Comment