Wednesday, August 16, 2023

UKUSANYAJI MAPATO BAGAMOYO WAONGEZEKA.

 


Na Mwandishi wetu- Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bi, Halima Okash ameipongeza Halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze kwa kuongeza ukusanyaji wa Mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika kikao cha Ushauri Wilaya kilicho fanyika ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo leo tarehe 16 Agosti 2023.


Pamoja na pongezi hizo Mhe, Okash amewataka Viongozi wa Halmashauri kuwa wabunifu katika kuibua vyanzo vya mapato na kutengeneza mikakati kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani kwakuzingatia haki na usawa.


”Bila mapato hakuna Halmashauri tunategemea mapato katika kujenga Hospitali, Shule, Barabara, na kusambaza huduma nyingine za kijamii ikiwemo maji, umeme”.Alisema Mhe, Okash.


Pia amewataka Maafisa Tarafa, Kata na Vijiji kuvumbua vyanzo vya mapato vitakavyo saidia kukuza na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao, vilevile amewaomba Maafisa hao kuhakikisha wanatatua kero za Wananchi hivyo kuwafanya wananchi hao kuwa huru na kuweza kuendelea na shughuli zao za maendeleo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe, Mohamed Usinga, ameziomba taasisi zilizopo Wilaya ya Bagamoyo ikiwemo TANESCO na DAWASA kushirikiana na Halmashauri kutekeleza kwa vitendo katika kutengeneza na kuboresha Miradi inayoendelea.


”Naziomba Taasisi zote ziboreshe ushirikiano na Halmashauri ili tuweze kutekeleza miradi pomoja na shughuli zote za kijamii zinazoendelea katika Wilaya yetu kwa kufanya hivyo mambo yetu yatakwenda vizuri na kwa wakati ili tuweze kuendana na kasi ya Mhe.Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan”.







No comments:

Post a Comment