Waziri
Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Wafanyabishara na Mabalozi wa Nchi
Mbalimbali hapa nchini kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati
miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Alikutana nao
Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
..............................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4
kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara
wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi
lililotokea Mkoani Kagera.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo
vya watu 17 hadi leo na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya
wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata
nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia
wahanga hao leo (Jumanne, 13 Septemba, 2016) Waziri Mkuu amewashukuru kwa
michango yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji.
Amesema tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Amesema tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili
za sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na tetemeko
hilo.
“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na
tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze
kuendelea na shughuli zao za kawaida,” amesema.
Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka
tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa
kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Mawaziri wengine walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo
ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.
Amesema Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na
Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya
CRDB kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti
hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.
Pia Waziri Mkuu amewapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa
kuamua kutoa posho zao za kikao cha leo kwa ajili ya kuchangia wahanga wa
tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.
Wakati huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil
wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya
miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha
siku 30.
Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda
na Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk.
Aziz Mlima.
No comments:
Post a Comment