Ibada ya hijja imemalizika rasmi
katika mji wa Makkah na Madina na mahujaji wa dini ya kiislamu zaidi ya milioni
2 kutoka nchi zipatazo 164 wameanza kurejea makwao walikotoka.
Ibada ya mwaka huu imekuwa ya mafanikio kwa kumalizika salama, hii ni
kutokana na Serikali ya Saudi Arabia kuwa na mipango madhubuti kwa kuimarisha
miundombinu, usafiri, ulinzi na usalama na kurekebisha dosari zilizojitokeza
mwaka jana.
Maeneo ya misikiti yote miwili ya Makkah na Madina yaliimarishwa na
yanaendelea kujengwa ikiwa ni pamoja na kupanuliwa ili kuongeza nafasi za
kutosha kufanyia ibada.
Mahujaji kutoka Tanzania wapatao 2,000 wako salama na wao ni miongoni mwa
walioshiriki katika ibada na sasa wako njiani kurejea Tanzania.
Hatua
zilizochukuliwa na mamlaka za ulinzi za Saudi Arabia ni pamoja na kuhakikisha
kuwa makundi ya misafara ya mahujaji hayagongani kati ya wanaokwenda na
wanaorudi, njia mbalimbali zilikuwa zikifungwa na kufunguliwa ili kuruhusu
misafara kwenda uelekeo mmoja bila kukutana.
Hatua hii ilisaidia kuepusha ajali
kama iliyotokea wakati wa ibada ya hijja ya mwaka 2015.
Habari hizi ni kwa mujibu wa Kamati ya Hijja ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment