Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatumia fursa hii kufafanua kwamba,
msimamo alioutoa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu mgogoro wa uongozi katika
chama cha CUF una maana kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa kwake
na pande mbili zinazosigana na kwa mujibu wa Katiba ya CUF toleo la 2014,
Msajili alijiridhisha kwamba, Profesa Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa
Taifa wa chama cha CUF, kwa sababu alitengua barua yake ya kujiuzulu kabla
haijakubaliwa na mamlaka yake ya uteuzi, kama inavyoelekeza ibara ya 117(2).
Aidha, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inaviasa vyombo vya habari
kufanya jitihada za kuelewa msimamo wa Msajili wa Vyama vya Siasa, badala ya
kuandika habari au makala zinazopotosha umma.
Hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatumia fursa hii pia,
kukanusha taarifa zinazoenezwa katika vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya
kijamii kwamba, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema kuwa, hakumrudishia Profesa
Lipumba Uenyekiti wa Taifa wa CUF, bali Profesa Lipumba kajirudisha mwenyewe
kinyemela. Habari hiyo siyo ya kweli, imepotoshwa kwa makusudi, Watanzania
wanapaswa kuipuuza.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inawaasa viongozi wa kitaifa wa chama
cha CUF, kusoma kwa makini msimamo uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa na
kuuheshimu, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, Msajili
wa Vyama vya Siasa anao wajibu wa kujiridhisha kwamba, mabadiliko yoyote
yaliyofanywa katika uongozi wa taifa wa chama cha siasa, ni halali na
yamefanywa na mamlaka halali kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama husika.
Sisty L.
Nyahoza
Kny: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
No comments:
Post a Comment