TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI.
Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu anatarajia kukabidhiwa
uenyekiti wa Shirikisho la wakuu wa Majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika
(SARPCCO) katika mkutano unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 Septemba, 2016 jijini
Arusha.
IGP Mangu atakabidhiwa uenyekiti huo kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi
wa nchi ya Msumbiji ambapo atadumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka
mmoja.
Mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa kamati tendaji za SARPCCO amabazo
zitakutana Septemba 14 na 15 mwaka huu ili kuandaa ajenda na
mapendekezo ambayo yatawasilishwa katika mkutano wa wakuu wa Polisi ambao
unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Katika mkutano huo mambo mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu
yatajadiliwa ikiwemo uhalifu wa kuvuka mipaka, pamoja na kuweka mikakati na
maazimio ya kufanya Oparesheni za pamoja zinazojumuisha nchi zinazounda
shirikisho hilo.
Vilevile, mkutano huo utajadili kwa kina utekelezaji wa maazimio
mbalimbali kupitia kamati tendaji za wakurugenzi wa upelelezi, kamati
tendaji ya sheria, kamati tendaji ya mafunzo na kamati tendaji ya mtandao wa
Polisi wanawake.
Aidha, suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama
nalo litajadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa
Majeshi ya Polisi kwa nchi za kusini mwa Afrika katika kukabiliana na uhalifu.
Mpaka hivi sasa umoja huo unaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania,
Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo(DRC), Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland,
Madagascar na Seychelles.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment