Tuesday, September 20, 2016

BAADHI YA MAENEO HALMASHAURI YA CHALINZE YAKABILIWA NA UHABA WA CHAKULA

unnamed
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na viongozi mbalimbali wa serikali mkoa,wilaya pamoja na halmashauri mkoani humo juu ya hali ya chakula kimkoa. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
..........................................


Na Mwamvua Mwinyi.

SERIKALI mkoani Pwani imesema halmashauri ya Chalinze inakabiliwa na upungufu wa chakula ambapo unahitaji tani 443 za chakula cha bure kwa ajili ya watu 8,491 kutoka kwenye kaya 1,698.

Aidha imesema pia kunahitajika tani 1,404 za chakula cha bei nafuu kwa watu 26,889 kutoka kwenye kaya 5,378.

Mbali ya hayo,baadhi ya vyakula vikuu vinavyopatikana sokoni kutoka mikoa mingine bei zipo juu ikiwemo mahindi,sembe,mchele,maharage na sukari.

Akizungumzia hali ya chakula katika msimu wa mwaka 2015/2016 na maandalizi ya kilimo kwa msimu wa 2016/2017 ,kwa baadhi ya viongozi wa serikali mkoa,wakuu wa wilaya,wabunge na wenyeviti wa halmashauri ,mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,alisema hali ya chakula kimkoa ni ya wastani.

Alisema halmashauri ya Chalinze imekubwa na upungufu huo kwa sababu iliathirika zaidi na uhaba wa mvua katika kipindi cha msimu uliopita.
Mhandisi Ndikilo,alielezea kuwa tathmini ya kina ya hali ya chakula imefanywa na wataalamu wa mkoa na kubaini upungufu huo wa tani 443 za chakula.

Alisema mkakati ili kukabiliana na tatizo hilo, halmashauri zinapaswa kuwa na mazao ya mkakati kulingana kiasi cha mvua ikiwa ni pamoja na Chalinze kutakiwa kutilia mkazo mazao ya muhogo na mtama na kujiwekea kampeni maalum ya ondoa njaa Chalinze(ONJACHA).

“Elimu kwa wakulima iendelee pia kutolewa juu ya kutambua umuhimu wa utunzaji wa chakula na kiasi cha chakula kinachohitajika katika kaya kwa mwaka mzima .Na hii itasaidia kuondokana na upungufu wa chakula ‘alisema mhandisi Ndikilo.

Alieleza kuna kila sababu ya watendaji wa vijiji kuhakikisha wanasimamia sheria ya nguvu kazi kuona kwamba vijana na watu wenye nguvu wanajishughulisha na shughuli za kilimo.

Mhandisi Ndikilo alizitaka halmashauri ziendelee kuhamasisha wananchi kun’goa visiki ili matrekta yatumike kikamilifu.

Alisema halmashauri hizo zisimamie kila kaya kulima ekari moja ya muhogo kwani uzoefu unaonyesha maeneo yanayozalisha muhogo kwa wingi hayakabiliwi na uhaba wa chakula.

Alisema ni matarajio yake endapo mikakati hiyo itazingatiwa na kusimamiwa kwenye msimu ujao wa  chakula hali itakuwa shwari.

Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alisema ,taratibu zinaendelea kufanyika ili kukabiliana na tatizo hilo kupitia ngazi husika hadi ofisi ya waziri mkuu.

Nae afisa tawala msaidizi uchumi na uzalishaji mkoani humo,Shangwe Twamala akizungumzia suala la mfumuko wa bei za vyakula vikuu,alisema bei za sokoni hadi kufikia agost mwaka huu mahindi yanauzwa kwa sh.1,000 .

Alisema kwa upande wa sembe ni sh.1,200,mchele 1,300 hadi 1,900,maharage 2,000 hadi 2,200 na sukari ni sh.2,200 hadi 2,400.

Twamala alisema utekelezaji na malengo msimu wa kilimo uliopita ,kilimo cha vuli na masika hakikuwa kizuri kutokana na uchache wa mvua hali iliyosababisha mazao kama mahindi kukauka licha ya hekta 154,100 zililimwa na kuzalisha tani 675,717 za chakula.

No comments:

Post a Comment