Waziri wa
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akizungumza na
wachezaji wa Serengeti Boys na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam
mara baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Congo-Brazaville iliyofanyika
katika Uwanja wa Taifa Septemba 18,2016 Serengeti ilishinda kwa jumla ya goli 3
kwa 2.
............................................
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye
ameahidi kutoa kiasi cha shilingi Millioni moja kwa kila goli
litakalofungwa na Serengeti Boys katika mechi ya marudiano nchini Congo
Brazaville.
Ametoa ahadi hiyo wakati akiongea na kuwapongeza wachezaji hao mara baada
ya kumalizika kwa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Serengeti Boys ya Tanzania na Congo
Brazaville uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya Watanzania wote nawapongeza kwa mchezo mzuri mliouonesha na
kuibuka na ushindi lakini bado mnatakiwa kujituma kama mlivyofanya katika mechi
hii na naahidi kutekeleza ile ahadi yangu ya laki tano kwa kila goli na nitatoa
tena kwenu Millioni moja kwa kila goli mtakalofunga Congo Brazaville.”Alisema
Mhe. Waziri Nape.
Kwa upande wa Kocha wa Timu hiyo Bw. Bakari Shime ameshukuru Waziri
na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo na
watahakikisha wanapata ushindi katika mechi ya marudiano kwani wameshayaona
mapungufu yaliyojitokeza na watayafanyia kazi wachezaji watakuwa tayari kuivaa
tena Congo Brazavile.
Aidha Nahodha wa Timu hiyo Bw. Issa Abdi Makame mbali na kuishukuru
Serikali kwa motisha inayotoa ameahidi kujituma zaidi kwa kushirikiana na
wenzake na kufuata maagizo kutoka Bechi la ufundi ili
kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa marudiano.
“Tunashukuru sana kwa motisha mnayotupa na sisi hatutawaangusha
tutajituma kadri ya uwezo wetu tupate ushindi tukiwa ugenini ili tuweze
kufuzu” Aliongeza Nahodha Makame.
Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa Miaka
kumi na saba (Serengeti Boys) inayowania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe
la mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana yatakayofanyika nchini Madagascar mwaka
2017 inatakiwa kupata ushindi ili kujihakikishia kufuzu kwa fainali hizo.
No comments:
Post a Comment