Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Bi. Mwanalingwe Shani Juma
akiwa na mwanane mchanga, Ngweshani Khatibu wakati
alipotembelea wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ya Mafia Septemba 24,
2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.............................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk
Beatrice Byalugaba kufanya uchunguzi na kubaini madaktari wa hospitali ya
wilaya ya Mafia wanaomiliki maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo na
kuwachukulia hatua.
Amesema ameshangazwa kukuta maduka ya dawa yanayomilikiwa na madaktari
nje ya hospitali hiyo kwani tayari Serikali ilishaagiza kuondolewa kwa maduka
ya madaktari karibu na hospitali wanazofanyia kazi.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 24, 2016) wakati
alipotembelea hospitali ya wilaya ya Mafia katika siku ya pili ya ziara yake
wilayani mafia.
Kuhusu tatizo la upungufu wa dawa hospitalini hapo amemuagiza Dk.
Beatrice kufanya utafiti wa aina ya magonjwa yanayowasumbua wananchi wa wilaya
hiyo ili wanapoagiza waagize dawa nyingi za kutibu magonjwa hayo.
Pia aliwataka watumishi wa hospitali hiyo wajitahidi kuwahudumia vizuri
wagonjwa licha ya uchache wao. Lengo ni kuhakikisha wanapunguza malalamiko
kutoka kwa wananchi.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa
Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupatiwa matibabu bure kwa
kipindi cha mwaka mzima.
Awali Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Joseph Mziba alisema mwamko wa
wananchi kujiunga na mfuko wa CHF ni mdogo jambo linalokwamisha upatikanaji wa
huduma za afya wilayani Mafia. Jumla ya wananchi waliojiunga na CHF ni
watu 6,000 kati ya watu 50,000.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Eric Mapunda
ameiomba Serikali kutoa kibali kwa halmashauri kununua dawa ambazo zinakosekana
MSD kwenye soko moja kwa moja bila ya kupitia utaratibu wa manunuzi.
“Kuna wakati tunakosa dawa MSD na kulazimika kununua kwa mawakala kwa
kufuata taratibu ya manunuzi. Tunalazimika kununua boksi moja la ambapo boksi
moja la panadol linauzwa sh. 20,000 na tukinunua moja kwa moja sokoni bila ya
kufuata utaratibu huo boksi hilo hilo tunalipata kwa sh. 8,000,”alisema.
Baadhi ya wananchi waliokuwepo hospitalini hapo walieleza malalamiko yao
kuhusu lugha chafu na dharau inayotolewa na baadhi ya madaktari na wauguzi.
No comments:
Post a Comment