Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa wa kwanza kulia, akitazama samaki aina ya pweza wakati
alipotembelea kiwanda cha samaki cha TANIPESCA eneo la Kilindoni wilayani
Mfia Septemba 24, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza mkuu wa wilaya ya Mafia mkoani
Pwani, Bw. Shaib Nnunduma pamoja na mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Eric
Mapunda kuimarisha doria kwenye eneo la bahari ili kuzuia uvuvi haramu.
Amesema vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika wilaya hiyo
vinapaswa kudhibitiwa haraka kwa sababu vinasababisha halmashauri hiyo kukosa
mapato na kushindwa kuboresha maendeleo ya wananchi.
Waziri mkuu ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti leo (Jumamosi, Septemba
24, 2016) wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Tanpesca na
alipowahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha
Kirongwe wilaya ya Mafia.
Amesema uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi na chanzo muhimu cha mapato
kwa wilaya ya Mafia na suala la uvuvi haramu linaathiri sana mapato ya
halmashauri hivyo ni vema wakaimarisha doria ili kukomesha vitendo hivyo.
“Lazima jambo hili lidhibitiwe. Uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu
mazingira ya chini ya bahari hivyo samaki wanashindwa kuzaliana kwa wingi.
Hakikisheni watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na
kuteketeza zana wanazotumia,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Alphakrust inayomiliki kiwanda cha
Tanpesca, Ganeshen Vedagiri amesema kampuni hiyo imeajiri watumishi 855 kati
yake 445 ni wakazi wa wilaya ya Mafia huku wanawake wakiwa 250.
Amesema wanajumla ya mabwawa 76 ya kufugia samaki aina ya kamba na kwa
sasa yanayotumika ni 30 na kila moja lina uwezo wa kuzalisha kilo 5,000 katika
siku siku 150 na kufanikiwa kuvuna tani 300 kwa mwaka.
Mkurugenzi huyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016.2017
wanatarajia kupata wastani wa sh. bilioni 120 katika mauzo ya nje na sh.
bilioni 62 kutoka katika mauzo ya ndani. Wanaltarajia kulipa kodi ya zaidi ya
bilioni 15 kwa mwaka huu.
Kwa upande wake Mohamed Gomvu ambaye ni Diwani wa kata ya Kirongwe na
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mafia alisema maeneo yaliyoathirika
zaidi na uvuvi haramu ni vijiji vya Ndagoni (Kiega), Kifinge, Chunguruma
(Tumbuju) na kisiwa cha Nyororo.
Amesema jambo linalokwamisha ukamatwaji wa uvuvi haramu ni kutokana na
watumishi kukosa uamini na kuvujisha siri kwa wavuvi hao hivyo wanashindwa
kuwanasa kwenye mitego yao.
No comments:
Post a Comment