Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na
Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China, Bw. He Liehui, ofisini
kwa Waziri Mkuu, jijini Dodoma, Januari 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza
na Mwenyekiti wa Kampuni ya Touchroad Group ya China, Bw. He
Liehui, ofisini kwa Waziri Mkuu, jijini Dodoma, Januari 19, 2019.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
.........................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameahidi
kupokea kundi la watalii wasiopungua 300 ambao wanatarajiwa kuwasili nchini
Machi, mwaka huu.
Watalii hao ni kundi la kwanza
miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili nchini katika mwaka 2019
chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya
Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.
Ametoa ahadi hiyo leo (Jumamosi,
Januari 19, 2019) alipokutana na Mwenyekiti wa Touchroad Group, Bw. Liehui He
na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Thomas Mihayo ofisini kwake Mlimwa,
jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada
ya kuelezwa na Bw. He huyo kwamba kundi hilo la watalii likiwa Djibouti
litapokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na likienda Zimbabwe, litapokelewa na
Rais wa nchi hiyo.
“Tanzania imeamua kuweka mkakati wa
kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na kukuza
utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya asili, wanyama, fukwe
za bahari na milima. Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa, unatoa fursa mpya ya
kutangaza vivutio vya nchi yetu,” amesema.
“Nitoe wito kwa Watanzania wanaoishi
maeneo ya jirani na vivutio vyetu, wachangamkie fursa ya ujio wa watalii hawa
katika maeneo mbalimbali. Wakifika Dar es Salaam, wanaweza kwenda Kigoma kuona
Ziwa Tanganyika, mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini, Arusha au vivutio vya
Zanzibar. Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa mbalimbali,” amesema.
Pia amesema amefurahishwa na wazo lao
la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu cha utalii (tourist hub) kwa makundi ya
watalii ambayo yatakuja Tanzania na baadaye kutoka Tanzania kwenda Lusaka,
Harare, Johannesburg na Djibouti.
Mwenyekiti huyo ambaye aliwasili
nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31 ambao unajumuisha waandishi wa
habari, wasanii, wanamuziki na watu mashuhuri.
Akiwa Beijing, China, wakati
akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na China
lililofanyika Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu alikutana na uongozi wa kampuni
ya TouchRoad ambayo ilionesha nia ya kutangaza fursa za utalii zilizopo hapa
nchini.
Ziara ya Bw. He ni sehemu ya
utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya kampuni ya TouchRoad na Bodi ya
Utalii ya Tanzania, Novemba 2018.
Mapema, Bw. He alimweleza Waziri Mkuu
nia ya kampuni hiyo kutekeleza makubaliano yao ya kutangaza vivutio vya utalii
vya Tanzania katika soko la China ili kuvutia watalii wapatao 10,000
waitembelee Tanzania katika mwaka 2019.
“Tumepanga kuleta watalii 10,000 kwa
mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la kuongeza idadi hiyo kwa asilimia 20 kila
mwaka kwa muda wa miaka mitano. Pia tuna lengo la kuitumia ndege ya ATCL ili
ilete watalii moja kwa moja kutoka Shanghai, China,” alisema.
Akielezea ujio wa kundi la kwanza la
watalii, Bw. He alisema kundi hilo litakaa Djibouti kwa siku moja, Tanzania
siku nne (tatu za kulala) na Zimbabwe siku tatu (mbili za kulala) na kisha
kurejea China.
Alisema wanapanga kila mwezi wawe na
kundi kubwa la watalii ambao watakuwa wanafikia Tanzania na kupelekwa nchi
nyingine kwa sababu Wachina wengi hupenda kufanya utalii kwa siku walau 10,
lakini wapelekwe maeneo matatu au manne tofauti kuona vivutio vya aina nyingine
badala ya kukaa sehemu moja kwa kipindi chote hicho.
“Watalii hawa wakija kwa siku tatu au
nne, wana uhakika wa kutumia dola za Marekani zaidi 2,000, wakienda eneo
jingine watatumia fedha pia, namna hiyo tuna uhakika wa kuongeza pato la Taifa,
lakini pia tuna uhakika wa kutengeneza ajira kwa Watanzania,” alisema.
No comments:
Post a Comment