Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman
Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa
ya siku 68 kwa halmsahauri nne kurejesha fedha za mradi wa
elimu(Equip)zilizotumika kinyume na utaratibu.
........................
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Halmashauri 33 kati ya
halmashauri 185 zimeweza kukusanya mapato ya ndani kwa kiwango cha asilimia 50
na zaidi ya makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 huku halmashauri 21 zikiwa
zimefanya vibaya kwa kusanya chini ya asilimi 20 ya makisio yake kwa mwaka.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo alipokuwa
akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa robo ya pili ya
mwaka.
Alisema katika Halmashauri 33 zilizokusanya
asilimia 50 na zaidi zimo Halmashauri za Majiji tatu zikiongozwa na Jiji
la Dodoma, Manispaa ni mbili zikiongozwa na manispaa ya Iringa, Halmashauri za
Miji nane zikizongozwa na Mji wa Geita na Halmashauri za Wilaya ni ishirini
zikiongozwa na Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
“Uchambuzi unaonyesha kuwa Katika
Majiji 6, Jiji la Dodoma linaongoza kwa kukusanya asilimia 59 ya makisio na
Jiji la Tanga limekuwa la mwisho kwa kukusanya asilimia 33 ya makisio” alisema.
Aidha Manispaa ya Iringa imeongoza
katika kundi la Manispaa kwa kukusanya asilimia 64 ya makisio ambapo Manispaa
ya Lindi imekuwa ya mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 20 ya
makisio.
Jafo aliongeza kuwa kwa upande wa
Halmashauri za Miji, Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kukusanya
asilimia 84 ya makisio na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho
katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 9 tu ya makisio,
Alisema Katika kundi la Halmashauri
za Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 78
ya makisio ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu imekuwa ya mwisho kwa
kukusanya asilimia 6 tu ya makisio.
Kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ya
mapato ya Halmashauri Jafo alibainisha Halmashauri iliyoongoza kwa kuwa
ni Jiji la Dodoma ambalo limekusanya Shilingi Bilioni 40.12 na halmashauri
iliyokusanya kiasi kidogo cha fedha ni halmashauri ya Wilaya ya Momba ambayo
imekusanya shilingi milioni 105.04.
Waziri Jafo pia alibainisha Mkoa
ambao Halmashauri zake zimekusanya mapato kwa kuzingatia wingi wa mapato kuwa
ni Mkoa wa Dar es salaam ambao kwa jumla halmashauri zake zimekusanya shilingi
bilioni 77.4 na Mkoa wa Mwisho ni Katavi ambao halmashauri zake zimekusanya
shilingi bilioni 2.4 tu.
Alisema katika Mkoa uliokusanya
vizuri kwa kuzingatia asilimia ya makusanyo ni Mkoa wa Geita Halmashauri
zake zimekusanya asilimia 56.4 ya makisio ya mwaka ukifuatiwa kwa karibu na
Mkoa wa Dodoma uliokusanya asilimia 55.9 ya makisio yake na Mkoa wa mwisho kwa
kigezo hicho ni Mkoa wa Mtwara ambao umekusanya asilimia 15 ya makisio yake ya
mwaka.
Wakati huo huo Waziri Jafo amewataka
wakurugenzi wote ambao Halmashauri zao hazikufanya vizuri katika ukusanyaji wa
mapato kwa kukusanya chini ya asilimia kumi ya makisio yake kwa kipindi cha
nusu mwaka kujieleza na kujitathimini na kuhakikisha wanaongeza bidii katika
suala la ukusanyaji wa mapato.
“Halmashauri 9 kati ya 10 zilizofanya
vibaya katika mwaka wa fedha uliopita zimefanikiwa kufanya vizuri katika
kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2018/19 kwa kukusanya zaidi ya asilimia 20 ya
makisio yake” alisema .
Waziri Jafo pia aliwaagiza
Wakurugenzi wote kuhakikisha takwimu zote za mapato katika mfumo wa LGRCIS
zinafanyiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa IFMS(Epicor) kwani
taarifa zote za mapato na matumizi ya fedha zinatakiwa kutolewa kupitia mfumo
huo.
Ulinganifu huu wa taarifa za mapato
umelenga kuonesha jinsi kazi za ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa inavyoendelea kusimamiwa vyema na takwimu hizi zinazotolewa
ni kwa mujibu wa taarifa zilizofanywiwa usuluhisho na kutumwa katika mfumo wa
IFMS(Epicor).
Katika mwaka wa fedha 2018/19
Halmashaurti zilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo
vyake vya ndani na hadi kufikia Disemba 31,2018 Halmashauri zimekusanya
shilingi bilioni 300 sawa na asilimia 41 ya makisio.
Kwa kipindi cha kwa mwaka 2017/18
halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 687.3 na hadi kufikia
Disemba,2017 halmashauri hizo zilikuwa zimekusanya sh bilioni 281.3 sawa na
asilimia 41 ya makisio.
Takwimu hizi zinabainisha kuwa kuna
ongezeko la Shilingi bilioni 18.7 kwa mwaka wa fedha 2018/19 ikilinganishwa na
makusanyo kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2017/18.
No comments:
Post a Comment