Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kasi ya kampuni ya KEC ya nchini India
ambayo imepewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika Kituo cha kupoza
umeme cha Zuzu, Dodoma ambacho kinaongezewa uwezo wa megawati 400, mbali ya
megawati 48 za sasa.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo leo
jijini Dodoma baada ya kufanya ziara ya kukagua vituo mbalimbali vya kupoza
umeme ikiwemo cha Msalato, Mnadani na Zuzu ambapo
aliambatana na Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent
Luoga, watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya
Nishati.
Hata hivyo, Dkt Kalemani ameeleza
kuwa, mkandarasi huyo anapaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi januari mwakani ili
kuweza kuboresha zaidi hali ya upatikanaji umeme jijini Dodoma ambapo kazi ya
uunganishaji umeme kwa wananchi inaendelea na hivyo kuongeza matumizi ya
nishati hiyo muhimu.
Dkt. Kalemani amesema kuwa,
mkandarasi huyo anafanya kazi tatu ambazo ni kushusha umeme kwa kV 400 katika
kituo hicho, kujenga kituo cha kupoza umeme cha uwezo wa megawati 400 na
kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Ameongeza kuwa, mkandarasi huyo
alianza kazi hiyo mwezi Machi mwaka 2018 ambapo gharama ya mradi huo ni Dola za
Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania,
Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
Aidha, baada ya kukagua vituo hivyo
vya kupoza umeme, Dkt Kalemani amewaagiza TANESCO kuhakikisha kuwa kila kituo
kinakuwa na fundi sanifu atakayekuwa kituoni kwa masaa 24 ili inapotokea
hitilafu ya umeme, iweze kutatuliwa kwa haraka.
Vilevile, Dkt Kalemani ameagiza kuwa,
kila kituo kiwe na vifaa vya ziada vya umeme badala ya kusubiri kuagiza vifaa
hivyo mara linapotokea tatizo hali inayopelekea wananchi kukosa umeme na
kueleza kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu atakagua utekelezaji wa agizo hilo
na Meneja ambaye hatatekeleza, atachukuliwa hatua.
Aidha ametoa agizo kwa TANESCO kuweka
walinzi katika miundombinu ya umeme kwani kumekuwa na matukio ya baadhi ya
wananchi kuhujumu miundombinu hiyo kwa namna mbalimbali ikiwemo kukata nguzo za
umeme na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiusika.
Katika ziara hiyo pia Waziri wa
Nishati alizungumza na wafanyakazi wa TANESCO katika kituo cha kupoza umeme
kilichopo mjini Dodoma ambapo pamoja na kuwapongeza kwa kazi wanazofanya,
alionya kuwa, katika mwaka 2019, mfanyakazi atakayeonekana amefanya uzembe
utakaopeleka kukosekana kwa umeme, atachukuliwa hatua.
No comments:
Post a Comment