Friday, January 18, 2019

MFUMO WA TTMS KUONGEZA UWAZI NA MAPATO SERIKALINI: DKT. MAGUFULI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia katika  hafla ya makabidhiano ya Mfumo wa Kudhibiti Mawasiliano ya Ndani na Nje ya Nchi (TTMS) iliyofanyika makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es salaam leo Januari 18, 2019
......................................

Rais Dkt John Pombe Magufuli ametaka mfumo mpya wa usimamizi na udhibiti wa  sekta ya mawasiliano nchini TTMS kutumiwa vizuri ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mtandao pamoja na kuongeza pato la Taifa.


Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya mfumo huo kati ya Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya SGS/GVG, Rais Magufuli amesema kuwa sekta ya mawasiliano ni sekta nyeti na ni muhimu kwa ujenzi wa taifa na kwa sasa inakuwa kwa kasi kubwa duniani kote.


“Sekta ya Mawasiliano ni sekta iliyonyeti na ni muhimu kwa watu wote duniani na kwa sasa inakua kwa kasi kubwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 5 wanatumia simu za mkononi duniani kote huku watu bilioni 3.9 wakiwa wanatumia vifurushi (data), lakini kwetu Tanzania watu 42,961,000 kwa sasa wanatumia simu huku 22,995,000 wakitumia kifurushi”, alisema Rais Magufuli.


Rais Magufuli alisema kuwa katika ukuaji wa kasi ya ajabu kwa matumizi hayo ya simu idadi ya upashanaji habari nao umeongezeka duniani kote huku mifumo ya uapatikanaji wa habari hizo ikiwa wazi kwa kila mtu kwa jambo lolote litakalotokea duniani lisipo ripotiwa kwenye Redio na Televisheni basi ni kwa njia ya mawasiliano kama Facebook, Whatsapp, Twitter na Instagram.


Akizungumzia faida za sekta ya Mawasiliano nchini Rais Magufuli alisema kuwa sekta ya mawasiliano ni kichocheo kikubwa cha uchumi kwa jamii kwani kwa sasa kinaongeza uzalishaji viwandani na duniani kote kwani teknolojia ya viwanda sasa inaendeshwa na sekta hii hasa kwa biashara za rejareja za mitandao yaani (E-Commerce).


“Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2017 biashara za rejareja zilizofanyika kwa njia ya mtandao yaani E-commerce zilikuwa na thamani ya trilioni 2.3 na hivyo kuzipita biashara za madukani na kwenye super market kwa hiyo watanzania mfumo huu mpya utaiongeza uwazi kwa biashara hiyo”, alisisitiza Rais Magufuli.


Katika mfumo huu wa mawasiliano huduma mbalimbali kama vile afya na elimu zinapatikana kwa njia ya mtandao yaani E-education na E- health, huduma za usafiri yaani Uber na taxify, lakini pia kupitia uwazi wa mfumo huu watu waliojisajili kwenye huduma za kifedha kwa sasa wanafikia watu milioni 20.85, kitu kilichochangia kwa Tanzania kuwa kinara wa uchumi jumuishi kwa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika.


Rais Magufuli alitaja sehemu za  mfumo huo ambao utaleta uwazi mkubwa kwa mawasiliano nchini katika Serikali ya Awamu ya Tano kuwa utakuwa ni mfumo wa kusimamia ubora wa mawasiliano Tanzania, kutoa takwimu za mawasiliano kwa njia ya sauti, matumizi ya  vifurushi vya simu na jumbe fupi na kubaini mawasilino ya simu za kimataifa zinazofanyika kwa njia ya udanganyifu.


Mifumo mingine iliyoko kwenye TTMS ni kufuatilia miamala ya kifedha inayofanyika kwa njia ya mtandano, kutambua namba tambulishi (IMEI) ya simu za kiganjani na kuhakiki kuwa vifaa vilivyounganishwa kwa watoa huduma zinakidhi kiwango cha kimataifa na mfumo wa mwisho TTMS ni ule wa kuhakiki mapato yatokanayo na simu/mtandao.


Aidha Rais Magufuli alieleza jinsi matumizi ya mfumo huo ulivyoleta faida tangu uanze kutumika ambazo ni kufahamu idadi kamili ya watumiaji wa simu na vifurushi, TTMS umepunguza kiwango cha udanganyifu kutoka asilimia 65 mpaka asilimia 10 sasa.


Katika kuweka bayana uwazi wa mawasiliano kupitia TTMS  Serikali imevuna fedha za kitanzania shilingi bilioni 93.665  huku shilingi bilioni 82.258 zikienda hazina na shilingi bilioni 11.407 zikipelekwa COSTECH, kwa hiyo kuongezeka kwa uwazi katika mawasiliano kwa kutumia TTMS imeweza kuongeza mapato kwa Serikali.


Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe alisema kuwa uwazi kwa kutumia mfumo wa TTMS umewezesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kwani kwa sasa sekta hii imekuwa pana zaidi nchini hasa kwa wamiliki wa laini za simu.


“Mfumo huu TTMS utaweka uwazi zaidi na kuchangia mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa taifa tangu kuanzishwa kwake 2017 kwani watumiaji wa simu za mkononi walionekena wakiongezeka kwa kasi kutoka 39,808,419  mwaka 2015 mpaka 42,661,449 mwaka 2018 hii inaonesha kuwa mfumo huu utakuza sekta ya mawasiliano kwa kasi zaidi kwa miaka ijayo hapa nchini”, Waziri Isack Kamwelwe.

No comments:

Post a Comment