Tuesday, January 1, 2019

DC BAGAMOYO AKABIDHI VITAMBULISHO KWA WAJASILIAMALI.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, akimkabidhi kitambulisho mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo, zoezi ambalo lilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa wilaya.
 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, akizungumza na wafanyabiashara ndogo ndogo.
................................................ 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wafanya biasahara ndogo ndogo kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wafanyabiashara hao kuzingatia vigezo villivyowekwa kwa mfanyabiashara anaestahiki kupata kitambulisho hicho.

Alisisitiza kuwa, mfanyabiashara atakaekiuka masharti yaliyowekwa na kusema uongo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, amewaagiza maafisa biashara na wale wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili wale wanokidhi vigezo waweze kupatiwa vitambulishi hivyo.

Katika hatua hiyo ya uzinduzi, Mkuu huyo wa wilaya amewakabidhi wafanyabiashara ndogo ndogo 10 wa awali ambapo baada ya hapo zoezi litaendelea kwa kushirikiana kati ya Maafisa wa biashara na wale wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na watendaji wa kata kwaajili ya kuwatambua wafanyabiashara ndogo ndogo wenye sifa ya kupata vitambulisho hivyo.

Tayari zoezi la awali limeshafanyika la kuwatambua wafanyabiashara ndogo ndogo ambapo mitaji yao haizidi milioni 4.

Katika hatua ya awali kwa Halmashauri ya Bagamoyo jumla ya wafanyabiashara ndogo ndogo 4,400 wamekidhi vigezo na kustahiki kupewa vitambulisho hivyo.

Kwa upande wao wafanyabiashara ndogo ndogo, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa hatua hiyo ambayo itawaondolea kero wafanyabiashara wadogo wadogo.

Walisema awali walikuwa wakisumbuliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) hata kama biashara ikiwa ndogo unatakiwa kukadiriwa kodi hali iliyopelekea watu wengi kushindwa kuendesha biashara zao.

Waliongeza kwa kusema kuwa, utaratibu huu wa sasa ni mzuri kwa upande wao kwani kila mmoja ataweza kuiingizia serikali mapato kulingana na uwezo wake.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogo ndogo nchini wenye mitaji isiozidi shilingi milioni nne 4,000,000/= ili waepukane na usumbufu wanaoupata kutoka TRA na mgambo wa jiji.

Jumla ya vitambulisho laki sita na sabini elfu 670,000 vilitolewa na kugawanywa kwa wakuu wa mikoa nchi nzima ambapo kila mkuu wa mkoa alipewa vitambulisho 25,000 avigawanye kwenye wilaya zake.
Baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo waliokabidhiwa vitambulisho vyao na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo.
Sehemu ya wafanyabiashara ndogo ndogo waliofika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kupata vitambulisho vyao.

No comments:

Post a Comment