Thursday, January 3, 2019

RPC MOROGORO AIPONGEZA TIF.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF).
..................................... 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa,  ameipongeza Taasisi ya The Islamic Foundation yenye makao yake makuu Mkoani humo kwa kazi inayofanya katika kuihudumia jamii.

Kamanda Mutafungwa amesema Taasisi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika shughuli zake ambazo zinafanywa na kusimamiwa kwa weledi huku huduma zake zikiwa hazibagui dini, rangi wala kabila.

Akizungumzia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Taasisi hiyo  Kamanda Mutafungwa amesema vyombo hivyo vimekuwa msaada mkubwa kwa jeshi la polisi mkoani humo kutokana na vipindi vyake vya kuelimisha jamii kuhusu amani, na usalama barabarani hali iliyopelekea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ajali za barabarani.

Aliongeza kwa kusema kuwa, vyombo vya habari vinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani mahali popote pale na kwamba vikitumika vizuri vinakuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kulinda amani ya sehemu husika.

Alisema jeshi la polisi linahitaji ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake hivyo kinachofanywa na Taasisi ya The Islamic Foundation ni kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kurahisisha utendaji kazi wa polisi.

Alifafanua kuwa, jeshi la polisi kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao huku wajibu wa raia ni kutii sheria bila ya shuruti na kwamba anaevunja sheria anachukuliwa hatua kwa mujibu wa kosa alilotenda.

Alisema katika hali hiyo, raia wakielewa kazi ya polisi, na wajibu wao wa kutii sheria kama raia, hakutakuwa na uhasama miongoni mwao na kwamba uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii utafanywa kwa ushirikiano.

Akizungumzia ajali za barabarani, Kamanda Mutafungwa amesema kwa sasa ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba utii wa sheria hasa kwa madereva wa bodaboda upo kwa kiwango kikubwa mkoani humo.

Alimalizia kwa kuwataka wananchi wote mkoani humo kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria, ikiwemo zile za barabarani na uhalifu wa aina zote.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref  Nahd amelipongeza Jeshi la polisi mkoani humo kwa kutoa ushirikiano wao na Taasisi hiyo hali inayaopelekea kuendesha vipindi vya usalama barabarani kupitia Tvimmaa na Redio imaan ambapo elimu hiyo imewasaidia sio tu wakazi wa mkoa wa Morogoro, bali kila sehemu vinaposikika vyombo vya habari vya imaan.

Alisema Taasisi hiyo pamoja na kujishughulisha na huduma za kiroho lakini pia inatekeleza miradi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuisaidia serikali katika kuleta maendeleo.

Aidha, Mwenyekiti Aref Nahdi,  alimueleza Kamanda Mutafungwa kuwa, Taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu mbalimbali kuhusiana na kulinda amani na kwamba katika hilo inashirikiana na wahadhiri mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kudumisha amani.

Aliongeza kuwa, wamefanikiwa kuandaa makongamano ya kuelimisha jamii umuhimu wa amani ndani ya mkoa wa Morogoro na nje ya mkoa huo na kwamba muitkio unakuwa mkubwa hali inayoashiria kuwa elimu iliyokusudiwa inafika ipasavyo.

Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Morogoro, alitembelea ofisi za The Islamic Foundation (TIF) zilizopo msamvu mjini Morogoro kwa kutambuana na viongozi wa Taasisi hiyo ambapo aliweza kukutana na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahd, Mkurugenzi Mtendaji wa Taassi hiyo, Sheikh Ibrahim Twaha, na Katibu Mkuu Haroun Rajab.

Akiwa katika ofisi za The Islamic Foundatio, Kamanda Mutafungwa alijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo huku kumbukumbu zikiwa makao makuu ya ofisi.

Miongoni mwa shughuli alizoweza kuona kumbukumbu zake ni pamoja na ujenzi wa Misikiti, uchimbaji wa visima, utoaji wa misaada mbalimbali, vituo vya kulelea watoto yatima na uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.

Kamanda Mutafungwa ameipongeza The Islamic Foundation kwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuahidi kushirikiana nao katika kipindi chake chote atakachokuwepo Mkoani Morogoro.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, akimsikiliza Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foudation (TIF), Aref Nahdi, alipotembelea Makao ya Taasisi hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, akiwa anazungumza na Tvimaan nje ya ofisi mara baada ya kumaliza kuzungumza na viongozi wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Makao makuu ya Taasisi hiyo iliyopo Msamvu Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Sheikh Ibrahim Twaha, (Kulia) Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa (katikati) Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi, (kushoto) wakiangalia kitabu cha utekelezaji wa miradi ya TIF.

 Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi, (kulia) akimkabidhi zawadi ya ngao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa (katikati) anaeshuhudia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Sheikh Ibrahim Twaha.
Katibu Mkuu wa The Islamic Foundation, Haroun Rajab (kulia) Mwenyekiti, Aref Nahd, (katikati) wakifurahia jambo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa.

No comments:

Post a Comment