Friday, January 18, 2019

CHALINZE WAKUSANYA MIL. 700 MWEZI DESEMBA

Na Omary Mngindo, Chalinze

HALMASHAURI ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kwa mwezi wa 12 mwaka 2018 imeweza kukusanya mapato kiasi cha sh. Mil. 700 kupitia makusanyo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Zikatimu ameyasema hayo juzi alipozungumza na wakazi wa Kitongoji cha Pingo, kikao alichokiandaa kuzungunzia mikakati ya elimu kwa wanafunzi waliokosa nafasi ya kuanza Kidato cha kwanza mwaka 2019.

Alisema kuwa mapato hayo yamegawanywa katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo elimu, afya, mifugo na nyinginezo, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

"Tunawaomba viongozi endeleeni kuwahamasisha vijana kuunda vikundi vya Ujasiriamali kisha kuvisajili ili viweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri yao, ambayo haina riba unalipa kulingana na unachokikopa," alisema Zikatimu.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kulipa na kusimamia malipo ya tozo mbalimbali zinazotakuwa kulipwa kulingana na sheria na taratibu kwani mwisho wa siku zinarudi katika shughuli za kimaendeleo kwenye maeneo yao.

"Katika nakusanyo yanayoendelea kukusanywa, sehemu yake ndio hizi sh. Mil. 132 ambazo tumeziingiza kwenye ujenzi wetu wa sekondari ya Kata ya Pera ambayo imeshaanza kujengwa hapa Pingo," alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Pingo Miraji Dibwe aliishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kusaidia juhudi zilizoanzishwa na wananchi wa Kitongoji hicho.

Nae Shabani Kiwamba akielezea kilimo cha kutokamilika kwa zahanati yao ambayo inataraji kuwa Kituo cha afya cha Kata, ambapo alisema ni cha miaka mingi pasipokuwepo dalili za kukamilika.

No comments:

Post a Comment