Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akiangalia zao la mahindi ambalo
linakaribia kukauka katika eneo la mradi wa Kilimo cha umwagiliaji cha Gereza
Songwe.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akisalimiana na Mkuu wa Gereza
Songwe, SSP. Peter Anatory alipowasili katika Gereza la Kilimo Songwe leo
Januari 25, 2019 kwa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Jeshi hilo
pamoja na kukagua mashamba ya kimkakati katika kuelekea kujitosheleza kwa
chakula cha wafungwa magerezani.
..................................
Na ASP Lucas Mboje, Mbeya
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike
amesema kuwa Jeshi la Magereza limeanza utekelezaji wa mpango wa miaka mitano
wa kuelekea kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa magerezani katika magereza
kumi (10) ya kimkakati likiwemo Gereza Songwe, lililopo Mkoani Mbeya ambalo
limelima hekari 750 za zao la mahindi.
Akizungumza na wanahabari leo mara baada ya kukagua mashamba
ya mahindi katika Gereza la Kilimo Songwe, Kamishna Jenerali wa Magereza,
Phaustine Kasike amesema kuwa lengo la ziara yake ni kujionea hali halisi ya
ufanikishaji wa jukumu walilopewa na Serikali katika kuhakikisha kuwa
wanazalisha chakula kwa wingi cha wafungwa waliopo magerezani.
Amesema kuwa Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo
imeingizwa katika utekelezaji wa mpango huo wa uzalishaji chakula cha wafungwa ambapo
kila Gereza la kimkakati limepangiwa malengo ya kulima mazao mbalimbali ya
chakula cha wafungwa ikiwemo mahindi, maharage na mpunga.
“Mpango huu ni lazima tuufanikishe, hivyo tayari
tumekwishajipanga na nguvu kazi ya wafungwa inatumika ipasavyo katika kufanya
kazi katika magereza hayo kama mlivyojionea leo hapa Gereza Songwe, pia
tunajitahidi kusimamia rasilimali nyinginezo tulizonazo katika maeneo yetu ya
magereza ili tuweze kutekeleza ipasavyo maelekezo ya Serikali”. Alisisitiza
Jenerali Kasike.
Aidha, Jenerali Kasike ameongeza kuwa kwa sasa Jeshi hilo
linakusanya rasilimali zilizopo na kutoa kipaumbele katika magereza
yakimkakati, ambapo katika kukidhi mahitaji ya nguvu kazi ya wafungwa, tayari
wafungwa kutoka sehemu mbalimbali nchini wamehamishiwa katika magereza yenye
mkakakati ili kuongeza nguvu kazi yakutosha katika maeneo hayo yenye
uzalishaji.
Akisoma taarifa ya Magereza Mkoa kwa Kamishna Jenerali wa
Magereza nchini, Mkuu wa Magereza Mkoani Mbeya, SACP. Luhende Makwaia amesema
kuwa Mkoa huo una jumla ya magereza matano ambayo yanatekeleza shughuli
mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya kilimo, likiwemo Gereza Songwe.
Kuhusu msongamano wa wahalifu, SACP. Luhende Makwaia amesema
kuwa magereza yote ya mkoa wa mbeya yanakabiliwa na tatizo la msongamano wa
wafungwa na mahabusu kutokana na ongezeko la uhalifu unaotokana na kuongezeka
kwa idadi ya watu pamoja na kukosekana kwa gereza moja la wilaya katika mkoa
huo.
Mkoa wa Mbeya una jumla ya wilaya sita(6) ambazo ni Mbeya
mjini, Mbeya Vijijini, Chunya, Rungwe, Mbarali, na Kyela. Katika wilaya hizo ni
wilaya tano(5) tu zina magereza, wilaya moja(1) ya chunya hakuna gereza hali
inayochangia uwepo wa msongamano wa wahalifu katika mkoa. Aidha, katika
magereza matano yaliyopo hupokea na kuhifadhi wafungwa na mahabusu katika mkoa
huo.
Muonekano
wa mashamba ya mahindi katika Gereza la Kilimo yakiwa yamestawi kama
inavyoonekana katika picha.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akikagua moja ya mashamba ya
mahindi ya Gereza Songwe alipofanya ziara ya kikazi katika Gereza hilo kabla ya
kuendelea na ziara yake Mkoani Rukwa leo Januari 25, 2019.
Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akitoa maelekezo kwa Maafisa
Waandamizi wa Magereza Mkoani Mbeya alipotembelea na kukagua mashamba ya
mahindi ya Gereza Songwe.
Kaimu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Jeremia Minja (katikati) akiwa katika picha
ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa
pili toka kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Mbeya.(Picha zote na Jeshi la Magereza).
No comments:
Post a Comment