Na Grace Semfuko-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo Januari 9,2019 amewaapisha viongozi
mbalimbali aliowateua Ikulu Jijini Dar Es Salaam na kuwataka kufanya kazi kwa
kuzingatia weledi.
Viongozi walioapishwa ni pamoja na
Waziri wa Madini Dotto Biteko, Makatibu Wakuu wa Wizara watatu, Manaibu
Makatibu wakuu wa Wizara wawili,Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Balozi pamoja
na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma na Makamishna sita wa Tume hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha
viongozi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alimtaka Waziri mpya wa
Madini Dotto Biteko kusimamia rasilimali za Madini kwa kuanzisha vituo vya
madini kwenye mikoa inayofanya shughuli za uchimbaji.
Rais alisema kumekuwa na changamoto
kubwa kwenye sekta ya madini ambapotaarifa zinaonyesha Tanzania
kuongoza katika uchimbaji wa Madini katika Nchi za Afrika Mashariki
lakini imekuwa na kiwango cha chini cha uuzaji wa madini kwenye nchi hizo
na kuhoji ni kwa nini kumekuwa na hali hiyo.
Ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango
kwa kushirikiana na Benki kuu ya Tanzania BoT kutenga fedha kwa ajili ya
ununuzi wa dhahabu kwa wachimbaji hatimaye iweze kuuzwa nje kwa fedha za kigeni
ili kuiongezea nchi pato la fedha hizo.
“Ripoti mbalimbali katika nchi za
Afrika Mashariki zinaonyesha Tanzania kuwa nyuma katika uuzaji wa dhahabu
wakati sisi ndio tunaongoza katika uchimbaji, kwa ripoti hii ni lazima
tujiulize tunakwama wapi? Dhahabu tunazochimba zinauzwa wapi? Soko lipo wapi na
tunalijua? Tunapouza tunapata fedha kiasi gani? Wizara ipo na wataalamu wake na
hapo ndio changamoto inapoonekana” Alisema Rais Magufuli.
“Ndio maana wanasema nabadilisha
badilisha viongozi, sitaacha kubadilisha na hata Biteko ukifanya vibaya
nitakutoa tu na nitaweka mtu mwingine, nafanya hivi kwa ajili ya maendeleo ya
Watanzania, sisi tumepewa dhamana lazima tuwatumikie Watanzania” alisema Rais
Magufuli
Alisema kwa muda mrefu dhahabu
imekuwa hainufaishi nchi ingawa sheria zimerekebishwa lakini bado kumekuwa na
changamoto kubwa na kuitaka Wizara ya Madini kusimamia bidhaa hiyo na pia
kushirikiana na wachimbaji wengine katika kudhibiti madini hayo muhimu kwa
Taifa.
Rais pia alitoa pungezi kwa Mkuu wa
Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro kwa kusimamia utoroshwaji wa madini
uliofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi ya
viongozi wa juu wa Jeshi hilo wanane wa Mkoa wa Mwanza.
“Nikupongeze IGP kwa kusimamia vyema
zoezi lile, na wale askari wafanyiwe uchunguzi na kuchukuliwa hatua ikibainika,
naomba vyombo vya habari muandike habari zenu kwa uhakika na sio kupotosha,
mfano kuna gazeti moja limeandika habari ya kupotosha kuhusiana na kukamatwa
kwa dhahabu ile mkoani Mwanza” alisema Rais Magufuli.
Rais pia aliwataka viongozi
aliowateua kushirikiana na kuacha migogoro mahali pa kazi na kwamba anatambua
baadhi ya maeneo ambayo viongozi hawaelewani na wakati mwiongine kutoleana
maneno yasiyofaa huku akitolea mfano kwenye maeneo ya Nyasa, Gairo na Manispaa
ya Dodoma.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliwataka viongozi walioapishwa
kushirikiana katika kuimarisha maendeleo ya wananchi na kwamba ofisi yake
itahakikisha wanapata ushirikiano wa kutosha.
Nae Spika wa Bunge Job Ndugai
alimwomba Rais Magufuli kuwapa likizi mawaziri angalau kwa muda ili waweze
kupumzika ombi ambalo Rais Magufuli alisema iwapo Watanzania hawana likizo
katika ujenzi wa Taifa na mawaziri wanatakiwa kufanya kazi bila
kupumzika.
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim
Juma nae alisema Mahakama itashirikiana na viongozi hao katika kuimarisha
uhusiano na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.
Viongozi 14 waliapishwa katika hafla
hiyo akiwepo Dotto Biteko kuwa Waziri wa Madini ambaye awali alikuwa Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ameapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Afya,maendeleo ya jamii,jinsia wazee na watoto, Dorothy Mwaluko ameapishwa na
kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na uwekezaji na Elius Mwakalinga
kuwa Katibu Mkuu Ujenzi.
Wengine ni Profesa Faustine Kamuzora
aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu, Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI na Dkt
Francis Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa
umma na utawala bora.
Aidha Rais pia aliwaapisha Viongozi
wa Tume ya Utumishi wa Umma akiwepo Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Steven
Bwana pamoja na Makamishna sita wa tume hiyo akiwepo George Yambesi, Yahya
Mbila, Daniel Ole Njoolay, John Haule, Hadija Ally Mohamed Mbarak pamoja na
Immaculete Ngwale.
No comments:
Post a Comment