Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akitoka Kituo Kikuu cha
Polisi cha mjini Bukoba mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo
hicho, leo, kwa kufuatilia utendaji kazi wao. Katikati ni Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, na kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoani
humo, ACP Raymond Mwampashe. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na mamia ya wananchi mjini
Bukoba Mkoani Kagera, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Uhuru,
Mayunga mjini humo, leo. Lugola licha ya kuwa amewataka waendesha bodaboda
wafuate sheria za usalama barabarani, lakini ametoa onyo kwa Polisi mjini humo
kuacha kuwakamata waendesha bodaboda wakiwa hawajavaa sare.
............................................
Na Felix Mwagara, MOHA-Bukoba.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola
amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Askari Polisi nchini kukamata pikipiki
wakiwa hawana sare za Jeshi.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika uwanja wa uhuru, Mayunga, mjini Bukoba Mkoani Kagera, leo,
Lugola alisema polisi wanapaswa kufuata utaratibu wa kijeshi hasa wanapokamata
vyombo vya moto na siyo kuvunja utaratibu.
Lugola aliongeza kuwa, bodaboda zinazovunja sheria
za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa
Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biasahara hiyo.
“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya
makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni
kuwaonea waendesha bodaboda,” alisema Lugola.
Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini
Bukoba na Tanzania
kwa ujumla wafuate sharia za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu,
kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.
Lugola ameanza ziara yake ya siku nane mkoani humo
akitembelea Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na
kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo
ndani ya Wizara yake.
Lugola mwaka jana alitoa maagizo kwa makamanda wa
mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi
nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi
wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.
Waziri Lugola tayari amemaliza ziara yake kwa
Wilaya ya Bukoba na Kesho ataanza ziara Wilaya za Misenyi, baadaye Karagwe,
Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Januari 8, 2019 atamalizia ziara yake Wilaya ya
Muleba ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi
waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi
la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,
pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano
gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa
waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao
nje ya Gereza.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsikiliza Mkazi wa mjini
Bukoba alipokuwa anaeleza kero yake mara baada ya Waziri huyo kuwaita wananchi
hao mbele waweze kutoa kero zao, mara baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi
hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Mayunga mjini
humo, leo. Lugola licha ya kuwa amewataka waendesha bodaboda wafuate sheria za
usalama barabarani, lakini ametoa onyo kwa Polisi mjini humo kuacha kuwakamata
waendesha bodaboda wakiwa hawajavaa sare.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Bashiru Ally, wakati alipoonana naye Uwanja wa
Ndege wa Bukoba, leo. Lugola yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi akitembelea
Wilaya zote, akisikiliza kero mbalimbali za watumishi wa Wizara yake pamoja na
wananchi mkoani humo.
No comments:
Post a Comment