Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wadau wa taasisi ya Baps Charity
baada ya kufanya ziara katika taasisi hiyo na kukagua maendeleo ya
ukarabati wa wodi mpya ya watoto jana katika taasisi hiyo Jinini Dar es Salaam.
Wodi hiyo inatarajiwa kuwa wodi ya kwanza kwa watoto wenye magonjwa ya moyo
Afrika Mashariki na kati.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza baada ya kufanya ziara fupi ya
kukagua maendeleo ya ukarabati wa wodi mpya ya watoto wenye magonjwa ya moyo
jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam. Kulia
ni Mkuregenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi na kushoto ni
Meneja wa Jengo la taasisi hiyo Bi. Flora Kassembe. Wodi hiyo inatarajiwa kuwa
wodi ya kwanza kwa watoto wenye magonjwa ya moyo Afrika Mashariki na kati.
..................................
Na: Genofeva Matemu – JKCI
Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete
(JKCI) imekuwa taasisi ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kuwa
na wodi pekee ya kuwahudumia watoto wenye magonjwa ya moyo bila kuwachanganya
na watu wazima.
Eneo la wodi hiyo lilitolewa mwaka
2017 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe
Magufuli alipokua akizindua Hospitali ya Mloganzila na kuiagiza Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kutoa sehemu ya jengo linalohudumia watoto kwa JKCI ili
watoto wenye magonjwa ya moyo waweze kuwa na wodi yao katika kuleta ufanisi wa matibabu
ya moyo kwa watoto hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kufanya
ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa wodi hiyo Waziri wa Afya Maendeleo
ya Jamaii, Jinsi, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alisema upatikanaji wa wodi
hiyo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha utolewaji wa matibabu ya moyo kwa
watoto ya kibingwa yanaendelea kuboreshwa hapa nchini.
“Kwa wodi za watoto wenye magonjwa ya
moyo peke yake kwa hapa Afrika Mashariki na kati hii ndio itakua wodi ya kwanza
inayowahudumia watoto bila kuwachanganya na watu wazima na hii italeta ufanisi
zaidi kwani nafasi ya kufanya makosa haitakuwepo kwasababu kutakuwa na
wataalamu wanaohudumia watoto tu” alisema Waziri Ummy
Waziri Ummy, alisema wodi hiyo
ambayo ukarabati wake umekamilika inatarajiwa kuwa na vitanda 32 na
chumba cha uangalizi maalum (ICU) kitakachokuwa na vitanda 15 jambo ambalo
litasaidia kuwafanyia upasuaji watoto wengi zaidi waliopo katika foleni ya
upasuaji na kuokoa maisha yao.
“Serikali ilitoa milioni 700 kwa
ajili ya ukarabati wa wodi hii na sasa kwa mara nyingine tena serikali imetoa
milioni 500 kukamilisha miundombinu ya ukarabati wa wodi hii. Nawashukuru sana
taasisi ya Baps Charity ambao nao wamewekeza milioni 800 katika
kuhakikisha kuwa wodi hii inakarabatiwa, serikali tutazidi kuunga mkono juhudi
hizi ” alisema Waziri Ummy.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prf. Mohamed, Janabi alisema kwa
shifti mbili za kliniki ya watoto zilizopo JKCI inaona wagonjwa wa moyo hadi
sitini kwa siku thelathini wakiwa ni watoto, hivyo kulikuwa na umuhimu wa
kuongeza wodi hiyo ya watoto.
Akizungumzia upasuaji wa magonjwa ya
moyo prof. Janabi amesema kuwa jumla ya wangonjwa 1356 wamefanyiwa upasuaji wa
kufungua kifua na bila kufungua kifua kwa mwaka 2018, hii kwa mwaka jana
ukiondoa Afrika kusini JKCI ndio hospitali iliyofanya upasuaji kwa wangonjwa wa
moyo wengi zaidi kuliko nchi yoyote ya Afrika.
“Wodi hii mpya ni kwaajili ya watoto
chini ya miaka 13 pekee na hii itatufanya kuwa taasisi ya kwanza Afrika
Mashariki na kati kuwa na jengo lenye kuhudumia watoto bila kuwanchanganya na
watu wazima “alisema prof. Janabi
No comments:
Post a Comment