Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt.
Bernard Kibesse akitangaza uamuzi wa Benki Kuu kuhamisha mali na madeni ya Bank
M kwenda Azania Bank Limited leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam
..........................................
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua
kuhamisha mali na madeni ya Bank M kwenda Azania Bank Ltd.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, amesema katika mkutano na waandishi wa habari
BoT jijini Dar es Salaam tarehe 15 Januari 2019 kwamba kwa sasa, Benki Kuu,
Azania Bank Ltd na wadau wengine wanaendelea kuandaa taratibu za kisheria za
kukamilisha mchakato wa uhamishaji wa mali na madeni ya Bank M kwenda Azania
Bank Ltd.
“Wateja wenye amana na wadau wengine
wa Bank M watataarifiwa tarehe ya kuanza kupata huduma za kibenki kupitia
Azania Bank Ltd,” alisema na kuongeza kuwa “wateja wenye mikopo wanatakiwa
kuendelea kulipa mikopo yao kulingana na mikataba yao.”
Katika mkutano ambao pia ulihudhuriwa
na Naibu Gavana (AIC), Bw. Julian Banzi Raphael, Dkt. Kibesse alisema, Benki
Kuu iliamua kuhamisha mali na madeni ya Bank M kwenda benki nyingine kama njia
ya kutatua matatizo ya benki hiyo ambayo imekuwa chini ya usimamizi wa Benki
Kuu tangu mwezi Agosti mwaka 2018.
Katika Naibu Gavana Kibesse amewahakikishia
wananchi kwamba Azania Bank Ltd “itakuwa na ukwasi wa kutosha kuweza
kuwahudumia wateja wake na wateja wapya kutoka Bank M baada ya kuchukua mali na
madeni ya benki hiyo.”
“Mtaji wa Azania Bank Limited unatarajiwa
kufikia kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 164 ambacho ni juu zaidi ya
mtaji wa shilingi bilioni 15 unaotakiwa kisheria,” alisema.
Naibu Gavana ameuhakikisha umma
kwamba Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kulinda maslahi ya wateja wenye amana
katika mabenki na kuimarisha uhimilivu katika sekta ya fedha nchini.
Benki Kuu ya Tanzania ilichukua
usimamizi wa Bank M Ltd mnamo tarehe 2 Agosti 2018 baada ya Benki Kuu, ambayo
inajukumu la kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kubaini kuwa
Bank M ilikuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na hivyo kushindwa kulipa madeni
yake.
Baada ya kuiweka chini ya usimamizi
wake, Benki Kuu ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Bank M
kwa muda wa siku 90 ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili
kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mnamo tarehe 2 Novemba 2018 Benki Kuu
iliongeza muda wa usimamizi kwa siku 60 ili kupata muda wa kutosha wa
kutathmini hali ya kifedha ya Bank M, ambayo ilikuwa ni hatua muhimu katika
utatizo wa matatizo ya Benki hiyo. Hatua hizo ndio zimefikisha hatua ya leo.
Bank M ilipewa leseni na kuanza
kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mwaka 2008, na kuwa miongoni mwa benki
zilizokua kwa haraka na kuwa na mali zenye thamani zaidi ya shilingi za
Kitanzania trilioni moja. Bank M ilikuwa na jumla ya matawi matano, matatu
yakiwa jijini Dar es Salaam na mengine mawili yakiwa katika majiji ya Arusha na
Mwanza.
No comments:
Post a Comment