Wednesday, January 9, 2019

JESHI LA POLISI PWANI LATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA.

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, katika kuukaribisha mwaka mpya, limetembelea kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho. 

Msaada huo umekabidhiwa na Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani ASP Festo kwa niaba ya Af Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Wankyo Nyigesa ni:- Dawa za chooni box 3, Sabuni za kuoshea vyombo box 2, Pampers box 3, Sabuni ya unga ndooo 2, Sukari kilo 50, Kalamu box 6, Sabuni ya miche box 5, Mafuta ya kupaka box 3, Mafuta ya kula lita 20, Madaftari katoni 1, Chumvi katoni 1, Juice katoni 1, Mchele kilo 100, Unga kilo100 na mbuzi wa 2. 

Mbali ya vitu hivyo, watoto hao waliweza kupatiwa flana za usalama barabarani na vipeperushi vya usalama barabarani na vya kupinga vitendo vya ukatili baada ya kuwa wamepatiwa elimu ya usalama barabarani na dawati la elimu kutoka ofisi ya mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani wakishirikiana na mabalozi wa usalama barabarani (RSA) pamoja na ofisi ya dawati la Jinsi Mkoa wa Pwani juu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuripoti vituoni pale wanapofanyiwa vitendo hivyo.

 Aidha, Dr wa Polisi aliweza pia kuonana na watoto wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kutoka katika kituo hicho na kuweza kuwapatia tiba, ambapo amefungua milango kwa uongozi wa kituo hicho kuwapeleka kwenye matibabu kwenye zahanati ya Polisi watoto wenye uhitaji maalumu wa kuonana zaidi na Daktari kwajili ya matibabu ya kina. 

Dr. Festo ameongeza ofisi yake itaweka utaratibu wa kupita na kuwajulia hali kila baada ya wiki mbili kituoni hapo ikiwa ni katika kujenga mahusiano bora baina ya Polisi na jamii yenye uhitaji maalum. 

Awali, akizungumza na viongozi wa kituo hicho cha Fadhila pamoja na watoto wanaolelewa hapo, Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani Mosi Ndozero-ASP ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Pwani limelenga katika mwaka 2019 kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi maalum na kufungua klabu za mabalozi wa usalama barabarani kwenye maeneo mbalimbali na kwa kuanzia wameamua kuendesha mafunzo ya usalama barabarani kwenye vituo vya watoto wenye uhitaji maalum kundi ambalo limekuwa likisahaulika kwa muda mrefu. 

Kadhalika, mbali ya utoaji wa elimu katika kituo hicho pamoja na utoaji wa msaada, Mkuu huyo wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani alitumia muda wake kula pamoja na watoto wa kitu hicho ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kituo hicho bi Suleiha amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa msaada wanaoendelea kukipatia kituo chake mara kwa mara. "Tunaomba mtufikishie salam zetu kwa viongozi wote wa Jeshi la Polisi kwa msaada wenu wa mara kwa mara katika kituo chetu, mbali ya kuwa mna majukumu mengi ya kufanya lakini mmekuwa mkisaidia sana jamii kama wazazi kwenye malezi ya watoto wetu hawa".

Vitu mbalimbali vilivyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani humo.
  
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Picha zote Na Jeshi la Polisi Pwani.

No comments:

Post a Comment