Wednesday, January 9, 2019

SERIKALI KUSAINI MIKATABA YA UBANGUAJI WA KOROSHO JANUARI 10

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza mpango wa serikali kusaini mikataba ya ubanguaji wa korosho wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
............................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Serikali imesema kuwa tarehe 10 Januari 2019 itasaini mikataba na wamiliki wa viwanda vya ubanguaji wa korosho waliojitokeza kwa ajili ya kubangua korosho za serikali za msimu wa mwaka 2018/2019 zilizonunuliwa na serikali kwa bei ya Shilingi 3300 kwa kilo.

Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 8 Januari 2019 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara.

Alisema kuwa hivi karibuni serikali ilitangaza kuwa korosho ghafi zote zitabanguliwa nchini hivyo utekelezaji wa jambo hilo umeanza, ambapo Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko itaingia mikataba ya ubanguaji.

Pamoja na wamiliki wa viwanda kupewa kazi ya kubangua korosho lakini pia serikali imewakaribisha wananchi kujitokeza kubangua korosho za serikali kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja. “Wananchi wenye uwezo wa kubangua tunawaomba waende Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo-SIDO) kwa ajili ya kujiandikisha ambapo mpaka sasa watu 126 kwa ajili ya ubanguaji na Tani 29 zimechukuliwa kwa ajili


ya kuanza kubanguliwa” Alisisitiza Mhe Hasunga

Katika mkutano huo Waziri huyo wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kushuhudia utiaji wa saini mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Chakula Duniani (WFP) wa Bilioni 21 zitakazoiwezesha NFRA kunua mahindi kwa wakulima hivyo kuimarisha soko la nafaka nchini.

Mhe. Hasunga alisema kuwa pamoja na kuanza ubanguaji kupitia SIDO lakini serikaliimeanza mchakato wa kukufua viwanda vya ubanguaji vya serikali na watu binafsi nchini ili kuongeza ajira kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vya wabanguaji wadogo wadogo.

Akizungumzia kuhusu swala la malipo ya korosho na uhakiki wa wakulima alisema kuwa tayari kiasi cha korosho ambayo imekusanywa kwenye maghala makuu ni Tani 203,938.3 wakati korosho iliyopo kwenye Vyama vikuu vya ushirika ni Tani 29,803.53 inayofanya jumla ya korosho yote iliyopokelewa kwenye vyama vya ushirika na maghala makuu kuwa Tani 233,741.83 sawa na asilimia 84.7 ya lengo lililowekwa la ukusanyaji katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani.

Kuhusu malipo ya wakulima alisema kuwa miamala ya malipo ambayo imefanyika ni 261,458 yenye jumla ya watu 203,569.

Aidha, vyama 490 vilimelipwa kati ya vyama 617, Alisema


Mkoa wa Mtwara jumla ya vyama 39 bado havijalipwa, Mkoa wa Lindi vyama vitano na Ruvuma viwili hivyo serikali imejipanga ndani ya wiki mbili vyama hivyo kuwa vimelipwa.

Waziri Hasunga amesema kuwa mpaka kufikia jana tarehe 7 Januari 2019 fedha ambazo zimeingizwa kwenye Account za wakulima ni zaidi ya Bilioni 257 huku ambazo tayari zimeingia kwenye Account za wakulima ni Bilioni 226.2 ambapo Zaidi ya Bilioni 30.7 zilizohakikiwa bado hazijaingizwa kwenye Account za wakulima kutokana na taarifa za baadhi ya wakulima hao kutofautiana majina ama vinginevyo. “Tunawaomba sana wananchi kwenda Benki kujiridhisha kama Account zao zinafanya kazi kwani


serikali ina fedha za kuwalipa wakulima wote wa korosho” Alisema

“Tena nisisitize kwa wale wanaofanya biashara ya korosho kinyume na utaratibu maarufu kama (Kangomba) wajisalimishe na kuomba radhi wenyewe kuliko kusubiri serikali iwabaini” Alisema

Vilevile, Mhe Hasunga alisema kuwa wizara yake imeweka mikakati mbalimbali ambapo hadi kufikia Januari 31 mwaka huu zoezi la uhakiki wa wakulima wanaostahili kulipwa liwe limekamilika ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wawe wamelipwa.

Pia amewataka wananchi kupuuza taarifa mbalimbali zizotolewa na baadhi ya wananchi wasiolitakia mema Taifa kupitia mitandao ya kijamii kuwa serikali hailipi wakulima badala yake amesisitiza kuwa serikali ina fedha za kutosha kulipa wakulima wa korosho isipokuwa kangomba wao hawatalipwa.
 Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo akifatilia mkutano wa Waziri wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya Korosho (CBT) Mkoani Mtwara,  leo tarehe 8 Januari 2019.

No comments:

Post a Comment