Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kupitia madaktari wake bingwa wa magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na Madaktari
Afrika na Shirika la Cardio Start wote kutoka nchini Marekani
wameanza kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku 12 kuanzia tarehe 07/01/2019 hadi 18/01/2019 kwa watu
wazima .
Matibabu yanayofanyika katika
kambi hiyo ni upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua.
Upasuaji wa bila kufungua kifua
unafanyika kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa wagonjwa
kuzibuliwa mishipa ya moyo iliyoziba (Percutaneous Coronary Intervention – PCI)
na kuwekewa vifaa vinavyosaidia kurekebisha mapigo ya moyo ambavyo ni
(Permanent Pacemaker na High powered devices CRT-P, CRT –D) .
Wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji ni
wale wenye matatizo ya moyo ambayo ni valve, mishipa ya moyo iliyoziba,
moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matibabu kwa watu wazima waliozaliwa na
matatizo ya moyo na wale wenye matatizo ya moyo yaliyotokana na ugonjwa
wa Kisukari.
Kambi hii inaenda sambamba na
utoaji wa elimu kwa madaktari na wauguzi pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi
kwa wageni na wataalamu wetu. Katika kambi hii tunatarajia kufanya upasuaji wa
kufungua kifua kwa wagonjwa 20 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 25.
Hadi jana tarehe 8/1/2019 jumla ya wagonjwa
nane wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na wagonjwa wanne wamefanyiwa
upasuaji wa kufungua kifua.
Hii ni kambi ya kwanza ya matibabu ya
moyo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019 na ni mara ya kwanza kwa shirika Cardio
Start kuja hapa nchini kufanya kazi na sisi.
No comments:
Post a Comment