Thursday, January 17, 2019

WAVUVI BAGAMOYO WALALAMIKIA KUPIGWA NA ASKARI WA DORIA WANAOFUATILIA LESENI ZA UVUVI NA UVUVI HARAMU.

 Wavuvi wa Samaki mjini Bagamoyo wamelalamikia kitendo cha kupigwa na askari wanaofanya doria kuzuia uvuvi haramu pamoja na kukamata boti za uvuvi ambazo hazina leseni za uvuvi.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ufukwe wa Bahari ya hindi mjini Bagamoyo, wavuvi hao wamesema wamepigwa na askari wanaofanya doria katika ufukwe huo bila ya kupewa nafasi ya kujitetea kwa maelezo.


Wamesema hata kama ni leseni kuisha serikali ilipaswa kuwafuata wavuvi kwa njia za kibinadamu na kuwapa tarehe ya mwisho kulipia leseni zilizoisha muda wake na sio kupiga watu ambao wengine sio wahusika wa boti za uvuvi.


Aidha, wamesikitishwa kuona walipa kodi wakipigwa bila ya kujali utu na mchango walio nao kwa taifa kwani si kwamba wamegoma kulipia leseni bali baadhi yao leseni zao za uvuvi zimeisha muda wake.


MAONI YA WANANCHI:


Wananchi mbali mbali waliotoa maoni yao kuhusu jambo hilo wamesema Doria hiyo imefanyywa bila ya kuzingatia weledi, na taratibu za kiutu kwani taharuki imekuwa kubwa miongoni mwa wananchi katika ufukwe wa bahari.


Wamesema ni kawaida ya binadamu kujisahau katika kutekeleza wajibu wake lakini kinachotakiwa kufanywa ni kuwakumbusha katika njia za kistaarabu bila kuleta vitisho.


Wamesema miongoni mwa wanaomiliki boti za uvuvi ni watu wazima wenye busara hivyo ilipaswa waambiwe kwamba leseni zao zimeisha ili waweze kuzilizpia upya.


Mzee maarufu mjini Bagamoyo Ally bin Nasiri amesema watu wa Bagamoyo ni wastaarabu askari hawakupaswa kutumia nguvu na kuwapiga, walipaswa kueleza operesheni inayoendelea inahusu nini kisha kusubiri wananchi watekeleze.


Mzee Ally Nasiri amesema kwa siku kadhaa shughuli za uvuvi katika Bahari ya hindi mjini Bagamoyo zimesimama ambapo hali hiyo imeathiri uchumi watu huku wengine wakiataraji kupeleka watoto shule kwa fedha zinazotokana na uvuvi.


Katiak hali hiyo Mzee Ally Nasiri ameiomba serikali inapofanya operesheni kama hizo kuwajulisha wananchi juu ya kile wanachokifanya na hatua gani za kuchukua ili kuepuka usumbufu kuliko kufika ghafla na kuvamia watu wanaohusika na wasiohusika.


WIZARA YA UVUVI 


Mwandishi wa habari hizi alifika wizara ya mifugo na uvuvi jijini Dar es Salaam ili kujua ukweli wa jambo hilo.


Mkurugenzi idara ya uvuvi kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magesa Bulayi amesema zoezi la kuhakiki leseni kwa boti za uvuvi pamoja na kudhiti uvuvi haramu ni la nchi nzima hivyo wananchi wanapaswa kufuata sheria.


Akizungumzia kipigo, Bulayi amesema zoazi hilo haliambatani na kipigo cha aina yoyote kwa maafisa wa serikali na kwamba swala la ukaguzi wa leseni hufanyika mara kwa mara.


Swala la ukaguzi wa leseni za uvuvi hufanyika mara kwa mara likienda sambamba na udhibiti wa uvuvi haramu ili kuepuka madhara ya yatokanayo na uvuvi haramu.


Afisa mwandamizi kutoka wizara ya Mifugo na uvuvi ambae hakutaka kuandikwa jina lake kwakuwa yeye sio msemaji wa wizara amesema maagizo yanapotolewa kwa watendaji wa serikali katika kutekeleza kila mmoja ana mtazamo wake na utashi wake.


Alisema yapo mambo yanayofanyika huko na maafisa wa serikali wizara haitambui na wala haikuwatuma kufanya hivyo.


Alisema katika swala la kuhakiki leseni haliusiani na kipigo vinginevyo kama kimetokea kitu tofauti ambacho askari anaona kutumia kupiga ndio njia sahihi ya kumtuliza muhusika hilo lipo nje ya maagizo ya wizara.

Hata hivyo alisema ni vyema wananchi wakajifunza kuzingatia sheria na kuacha mazoea kwani katika kurekebisha mazoea kwenye jamii kuna athari zinazopatika kwa wanaorekebishwa.


Alisema hakuna mtu asiyefahamu madhara ya kuvua samaki kwa kutumia mabomu na matumizi ya nyavu ndogo na zile zinazoharibu makazi ya samaki.


Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha serikali inadhibiti uvuvi haramu zipo sheria zimetungwa ambazo zikizingatiwa zitalinda samaki na tutaweza kuzuia madhara yatokanayo na uvuvi haramu.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI ATOA TAMKO.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma leo wakati akiagiza wavuvi wote waliokamatwa waachiwe huru.
....................................................


Serikali imeagiza wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa la kutohuisha leseni zao za Uvuvi na vyombo vyao kwa mwaka 2019, waachiwe na makosa yao yafutwe mara moja.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Amesema kuwa Wizara yake juzi ilipata tarifa kutoka vyombo vya habari kwamba wavuvi katika ukanda wa Pwani bahari ya hindi hususani soko la feri Dar es saalam, na Bagamoyo hawakwenda kuvua samaki kwasababu ya kosa la kutokuwa na leseni za vyombo vyao na za uvuvi kwa mwaka 2019.


Kutokana na hali hiyo Ulega aliagiza kuwa wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa hilo kote nchini kuachiwa mara moja kuendelea na shughuli zao huku akiwataka maafisa uvuvi kutoka katika ofisi zao na kuwafuata katika mialo mbalimbali ili kuwakatia leseni.


“Kwa kuzingatia kuwa hiki ni kipindi cha mwanzo wa mwaka ambapo leseni zinatolewa Wizara inaelekeza kwamba wavuvi wote waendele kukatiwa leseni hadi Januri 31, 2019″amesisitiza Ulega.


Hata hivyo amewaagiza maafisa wote wa Wizara na Halmashauri katika kipindi hiki wawafuate wavuvi kwenye mialo ili kuwakatia leseni wenye sifa kulingana na sheria na kanuni za uvuvi.


Ulega amesema  kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inalojukumu la kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi nchini zinasimamiwa, kuhifadhiwa na kuvunwa kwa kuzingatia sheria ili ziwe endelevu.
“Kazi hii inapaswa kufanyika kwa kushirikiana na Halmashauri nchini na wadau wa Uvuvi’alisema.


Amesisitiza  kuwa katika kutekeleza jukumu hilo Wizara imekuwa ikiendesha oparesheni dhidi ya Uvuvi haramu na biashara haramu ya samaki na mazao yake kwa takribani kipindi cha mwaka mzima.


“Shughuli za uvuvi zinatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 pamoja na sheria nyingine za nchi.


“Kwa kuzingatia hilo kila mtu anayehusika na shughuli za uvuvi anatakiwa kuwa na leseni halali ya uvuvi na na leseni ya chombo anachotumia kwajili ya Uvuvi”alisema Ulega.


Amesema kuwa  Serikali inatoa wito kwa wavuvi wote kuzingatia sheria ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
 
Wavuvi wa Samaki mjini Bagamoyo wakiwa katika ufukwe wa Bahari wakiangalia mazingira mara taharuki kufuatia Doria inayodhibiti uvuvi haramu na ufuatiliaji wa leseni za uvuvi.
 
Wavuvi wa Samaki mjini Bagamoyo wakizungumza na waandishi wa habari katika ufukwe wa Bahari ya hindi Bagamoyo.

 Jengo la wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo jijini Dar es Salaam ambapo Mwandishi wa habari hizi kupata kauli ya wizara kuhusu kile kinachoendelea  Bagamoyo kuhusu operesheni ya kufuatilia leseni za uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu.
  

No comments:

Post a Comment