Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Balozi wa Uholanzi nchini
Mhe. Jeroen Verheul pamoja na wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakiwa
katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kwa ziara ya Mhe. Balozi
ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa
wananchi.
....................................
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
imepongezwa kwa jitihada zake inazozifanya za kuweza kuwafikia
wananchi wengi kwa kutoa huduma bora za matibabu, elimu na ushauri
wa jinsi ya kuepukana na magonjwa ya moyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa
Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul alipokuwa akiongea na
wafanyakazi wa Taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kuangalia huduma mbalimbali
za matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wagonjwa.
Mhe. Verheul alisema Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete ni moja ya Taasisi zinazofanya kazi vizuri ya kutoa huduma
ya matibabu ya moyo katika nchi zilizopo Kusini mwa Afrika .
Kuhusu Ubalozi wake
kushirikiana na Taasisi hiyo katika utoaji wa huduma kwa wananchi alisema
ataangalia ni jinsi gani watashirikiana katika programu mbalimbali
za afya ambazo zinatolewa hapa nchini kupitia Ubalozi wa Uholanzi.
“Wiki tatu zijazo nitaenda nchini
Uholanzi ambako tuna mkutano wa mabalozi wote. Kupitia mkutano huo nitaangalia
ni Taasisi ipi ambayo itaweza kuja nchini kufanya matibabu ya moyo kama
ilivyokuwa kwa nchi zingine ambazo zinatuma wataalamu wake kuja katika
Taasisi hii kutoa huduma za matibabu kwa wananchi”,alisisitiza Mhe. Verheul.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Mhe. Balozi kwa kuwatembelea
na kuona huduma mbalimbali wanazozitoa na kusema kuwa wanajitahidi
kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika Taasisi hiyo anapata huduma bora za
matibabu ya moyo.
Alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa
katika Taasisi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka ukilinganisha na miaka ya
nyuma hii inaonyesha kuwa hivi sasa wananchi wenye matatizo ya moyo wanaelewa
ni wapi pa kwenda kutibiwa magonjwa hayo.
“Kutokana na wataalamu wetu kuwa na
utaalamu wa kutosha na hospitali kuwa na vifaa vya kisasa tumeweza kufanya
upasuaji kwa wagonjwa wengi zaidi kwa mwaka 2018 ukilinganisha na mwaka 2017”.
“Mwaka 2018 tumefanya upasuaji wa
kufungua kifua kwa wagonjwa 1053 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 405 ambapo
mwaka 2017 tulifanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 225 na bila
kufungua kifua kwa wagonjwa 800”, alisema Prof. Janabi.
Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Balozi
Verheul alitembelea maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya
moyo (Cath Lab), jengo jipya la watoto ambalo ukarabati wake ukikamilika
litakuwa na vitanda 32 na vitanda tisa katika chumba
cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi ya watoto na wagonjwa
waliofanyiwa na wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua,
chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi
maalum (ICU).
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi
Robert Mallya akiongea jambo na Balozi wa Uholanzi nchini
Mhe. Jeroen Verheul wakati balozi huyo alipotembelea Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu
ya moyo wanazozitoa. Kushoto ni Mhandisi wa umeme wa Taasisi hiyo
Victor Kaduma.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
Sulende Kubhoja akisalimiana na Balozi wa Uholanzi nchini Mhe.
Jeroen Verheul wakati balozi huyo alipotembelea Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo
wanazozitoa. Katikati ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma ya Uuguzi
Robert Mallya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimweleza Balozi wa Uholanzi nchini
Mhe. Jeroen Verheul jinsi maendeleo ya ukarabati wa wodi ya watoto
unavyoendelea wakati balozi huyo alipotembelea JKCI kwa ajili ya kuona
huduma mbalimbali za matibabu ya moyo wanazozitoa. Ukarabati wa jengo
hilo ukikamilika litakuwa na vitanda 32 na vitanda tisa katika
chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiagana na Balozi wa
Uholanzi nchini Mhe. Jeroen Verheul mara baada ya balozi huyo
kumaliza ziara yake ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na
Taasisi hiyo kwa wananchi.
Picha na JKCI
No comments:
Post a Comment