Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akielezea jambo mbele ya Waandishi wa Habari
kuhusu hali ya Huduma za Afya mwaka 2018, tukio lililofanyika katika ukumbi wa
Wizara ya Afya jijini Dodoma.Waziri wa Afya,
..................................
Na WAMJW – DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Sekta ya Afya nchini yaendelea kukua kwa kasi, kutokana na Serikali kuendelea kuboresha Huduma kwa Wananchi zikiwemo upatikanaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, huduma za chanjo, huduma za afya ya uzazi na mtoto na Huduma za Dharura.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati
akitoa tamko mbele ya Waandishi wa Habari na baadhi ya viongozi wa Wizara,
kuhusu hali ya Huduma za Afya mwaka 2018, katika ukumbi wa Wizara ya Afya
jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuwa Katika mwaka
2018, jumla ya wajawazito 2,086, 930 walihudhuria na kuandikishwa Kliniki,
ikilinganishwa na wajawazito 2,009,879 Mwaka 2017, huku mwongozo wa utoaji
huduma za afya ya uzazi na mtoto unaelekeza wajawazito kuanza huduma mapema
kabla ya majuma 12 ya ujauzito na kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika
kipindi cha ujauzito.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa,
Katika kipindi cha mwaka 2018 jumla ya watoto 1,568,832 walizaliwa
ikilinganishwa na Watoto 1,498,488 mwaka 2017, huku wakipatiwa huduma
mbalimbali za chanjo ili kuzuia magonjwa yanayowaathiri Watoto ikiwemo ugonjwa
Kupooza, Kuharisha, Pepopunda, Pneumonia, homa ya ini na Surua.
“Katika kipindi cha mwaka 2018 hali
ya chanjo kwa Watoto nchini imeendelea kuwa katika kiwango cha juu zaidi ya
asilimia 85 ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kama
inavyoonyeshaa katik hapa chini” Alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo nWaziri Ummy amesema mwaka
2018 kumetokea jumla ya vifo 20,087 ikilinganishwa na vifo 19,693 mwaka 2017,
huku Katika kipindi cha miaka yote miwili 2017 na 2018, homa ya mapafu
imeongoza kwa kusababisha vifo, ambapo kwa mwaka 2017, imechangia asilimia 18.2
ya vifo vyote na mwaka 2018 imechangia kwa asilimia 12.9 ya vifo vyote.
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa
Mwaka 2018, ugonjwa usio wa kuambukiza (shinikizo la damu) umejitokeza katika
magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo ambapo umechangia vifo kwa
asilimia 1.9 ya vifo vyote.
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy
amesema kuwa Hali ya upatikanaji wa Dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma
za afya nchini imeendelea kuimarika, hii ni kutokana na Serikali kuongeza
bajeti ya dawa kutoka Shilingi Milioni 31 mwaka 2015/16 hadi kufikia Shilingi
milioni 251 mwaka 2016/17 na Shilingi 270 mwaka 2018/19.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa hali
ya upatikanaji wa Damu Salama ambapo katika kipindi cha mwaka 2018, huku jumla
ya chupa za damu salama 307,835 sawa na asilimia 85.5 ya lengo zilikusanywa
ikilinganishwa na chupa 233,933 mwaka 2017, huku akiwahasa Wananchi kujitokeza
kuchangia damu ili kuendelea kuokoa maisha ya wahitaji.
“Chupa zote 307,835 zilizokusanywa
zilipimwa makundi ya damu pamoja na magonjwa makuu manne ambayo ni Ukimwi
(HIV,) Homa ya Ini B na C (HBV, HCV) na Kaswende (Syphilis). Jumla ya chupa
262,283 sawa na asilimia 85.3 zilikuwa salama na kusambazwa katika hospitali
kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.” Alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa,
katika mwaka 2018 jumla watu 47,967 waligundulika kuwa na vijidudu vya Kifua
kikuu ikilinganishwa na wagonjwa 44,714 waliogunduliwa mwaka 2017., huku
akisisitiza kuwa tatizo la ugonjwa wa Kifua Kikuu limeendelea kuwepo takribani
mikoa yote nchini.
kwa upande mwingine, Waziri Ummya
amesema kuwa, hadi kufikia Desemba 2018, jumla ya vituo vya kutolea huduma za
Afya vilifikia 7,768 kutoka vituo 7,435 mwaka 2017 sawa na ongezeko la vituo
333 kwa mwaka, amedai kuwa Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 71 ya vituo vya
kutolea huduma; Mashirika ya dini asilimia 12, Taasisi za Serikali asilimia 3
na vituo binafisi asilimia 15.
No comments:
Post a Comment