MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,
imemwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC), Tido Mhando baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha shitaka
dhidi yake.
Tido alipanda kizimbani jana
mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi MKuu Huruma Shaidi, wakati shauri hilo
lilipopelekwa kwa ajili ya kusomewa hukumu.
Mshitakiwa huyo alikuwa anakabiliwa
na mashitaka manne ya kutumia madaraka vibaya likiwemo la kuisababishia
Serikali hasara ya sh. milioni 887.1.
Akisoma hukumu hiyo jana na Hakimu
Shaidi, alisema upande wa mashitaka wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo
ulipeleka mashahidi watano ambao walishindwa kuthibitisha shitaka hilo.
Hakimu Shahidi alisema kutokana na
upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka hivyo anamwachia huru.
Awali, akichambua ushahidi huo,
alisema Tido kipindi akiwa Mkurugenzi wa TBC aliingia mkataba wa makubaliano na
Channel 2 kwa kuibadilisha TBC kutoka analogi kwenda digital.
Alisema mshitakiwa huyo alisaini
mkataba huo yeye peke yake bila ya uongozi wa shirika hilo wala wakili.
Aliendelea kuchambua ushahidi huo
alisema mkataba huo inadaiwa ulikuwa sio wa halali kwani yalikuwa ni
makubaliano ya awali.
Pia mkataba huo ulikuwa hauna ligo ya
TBC na haukuwa na nguvu kisheria.
Upande wa mashitaka unadai mkataba
huo haukufuata utaratibu wa kisheria.
” Kwali mkataba kuitwa mkataba lazima
ukamilike lazima kuwepo na watu ambao wanahusika na lazima kuwepo na
mwanasheria hivyo mkataba huo sio halali bali ni makubaliano ya awali, ”
alisema.
Baada ya uchambuzi huo, Hakimu Huruma
alisema mshitakiwa huyo hakuna sehemu ilithibitisha kwamba ulikuwa ni mkataba
hivyo anamwachia huru.
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa(TUKUKURU), Leonard Swai, baada ya uamuzi huo, aliambia
mahakama kwamba ana nia ya kukata rufaa.
Mshitakiwa alikuwa anatetewa na
wakili Dk. Ramadhani Maleta.
Miongoni mwa mashahidi wa upande wa
mashitaka waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni pamoja na Afisa uchunguzi wa
TAKUKURU, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu
mstaafu wa TBC, Clement Mshana.
Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16,
mwaka 2008, akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa
Mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini
mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na
Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni
kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Katika shitaka la pili, Tido anadaiwa
kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, mwaka 2008 aliposaini makubaliano kwa
utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shitaka la tatu, anadaiwa
Agosti 11, mwaka 2008 na Septemba mwaka 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya
madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga
vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha
BVI.
Katika shitaka la nne, anadaiwa kuwa
Novemba 16, mwaka 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini
mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast
Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika shitaka la mwisho, anadaiwa
kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, mwaka 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia
TBC hasara ya sh.887,122,219.19.
No comments:
Post a Comment