Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu hali ya Mfumuko wa Bei kwa mwezi Desemba 2018 leo jijini
Dodoma.
..........................................
Na: Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa
kutoka Januari hadi Desemba Mwaka 2018 umepungua hadi asilimia 3.5 kutoka
wastani wa asilimia 5.3 kama ilivyokuwa mwaka 2017.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Bw. Ephraim Kwesigabo wakati akitoa taarifa kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi
Desemba 2018 pamoja na wastani wa mfumuko huo kwa mwaka mzima.
“Wastani huu wa mfumuko wa bei wa
mwaka wa asilimia 3.5 ndiyo wastani mdogo kabisa kwa kipindi cha zaidi ya miaka
40 iliyopita ambapo tangu mwaka 1970 mfumuko huo ulikuwa 3.6,” ameongeza
Kwesigabo.
Aidha, akizungumzia kuhusu mfumuko wa
bei wa Taifa kwa mwezi Desemba ,2018, Kwesigabo amesema kuwa mfumuko huo
umeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.0 kwa mwezi Novemba
2018.
“Kuongezeka kwa Mfumuko wa bei wa
Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2018 kumechangiwa hasa na kuongezeka
kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi
kilichoishia mwezi Desemba, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba, 2017,
mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Desemba, 2018
umeongezeka hadi asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.4 ilivyokuwa mwezi Novemba,
2018,” amefafanua Kwesigabo.
Aidha amesema kuwa, baadhi ya bidhaa
ya chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nyama kwa
asilimia 4.6, samaki wabichi asilimia 8.2, dagaa asilimia 26.2, matunda kwa
asilimia 4.3 na mbogamboga asilimia 8.5 baadhi ya bidhaa zisizo za chakula
zilizochangia mfumuko wa bei ni pamoja na vitambaa vya kushonea nguo kwa
asilimia 2.1, nguo za kiume na za kike kwa asilimia 6.1, nguo za watoto kwa
asilimia 3.0, sare za shule kwa asilimia 3.1, dizeli kwa asilimia 27.6, petroli
asilimia 10.8 na huduma za malazi kwa asilimia 6.8.
Kwa upande wa nchi za Afrika
Mashariki, mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018 nchini Kenya
umeongezeka hadi kufika asilimia 5.71 kutoka asilimia 5.58 kwa mwaka ulioishia
mwezi Novemba, 2018 na mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018
nchini Uganda umepungua hadi kufika asilimia 2.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka
ulioishia mwezi Novemba, 2018.
No comments:
Post a Comment