Wednesday, January 2, 2019

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA LEO

Jeshi la Poliisi Mkoa wa Mwanza kwa kutumia kikosi chake kabambe chenye uweledi uliotukuka tumefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 110, huko mtaa wa Ngumo “A”, Wilayani Kwimba.

Tukio hilo limetokea tarehe 01.01.2019 majira ya saa 21:00hrs, hii ni baada ya kikosi hicho mahiri cha askari wakati kikiwa doria na misako kilipokea taarifa toka kwa wasiri kwamba katika mtaa wa Ngumo ”A” na Safari club wapo watu wanaojihusisha na utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya. 

Ndipo askari walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu wakiwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya aina ya bhangi.

Watuhumiwa waliokamatwa na dawa hizo za kulevya aina ya bhangi ni;

Consolatha Elias, miaka 52, mkazi Ngumo “A”, huyu amekamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 100.

Emmanuel Lucas, miaka 21, mkazi wa kijiji cha Manguluma, na
Rehema Joseph, miaka 27, mkazi wa Chato, hawa wawili wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 10.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea na mahojiano na watuhumiwa wote watatu ili kuweza kubaini watu wanaoshirikiana nao katika uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa hizo za kulevya aina ya bhangi. Aidha pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya wananchi waojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuwa waache kwani ni kinyume na sheria na endapo mtu atabainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. 

Vilevile tunawaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutupa mapema taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Imetolewa na;

Jonathan Shanna – ACP
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.
02 January, 2019.

No comments:

Post a Comment