Benki
Kuu ya Tanzania imetoa tangazo kwa umma kupitia tovuti yake (www.bot.go.tz)
likiwataka watu na taasisi zote zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha
zilizoko Tanzania Bara (isipokuwa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo –
SACCOS) kutoa taarifa zitakazotumika katika utayarishaji wa Kanuni za Usimamizi
wa Huduma Ndogo za Fedha. Taarifa hizo zinatakiwa kutumwa Benki Kuu ya Tanzania
hadi tarehe 31 Januari 2019.
Benki
Kuu inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tangazo hilo:
1.
Lengo la
tangazo hilo siyo kuvifunga au kuvibana vikundi vya kijamii kama VICOBA,
watu binafsi na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kama ambavyo
inapotoshwa na baadhi ya watu na mitandao mbalimbali ya kijamii, bali ni
kukusanya taarifa za awali kuhusu huduma hizo.
Kama ilivyoainishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupitisha Sheria ya Huduma Ndogo za
Fedha ya mwaka 2018, lengo la sheria hiyo ni kuwalinda wadau wote
wanaohusika na huduma hizi (watoaji na watumiaji) kwa kuziwekea utaratibu mzuri
zaidi wa uwekaji kumbukumbu, uendeshaji na uongozi kwa ujumla. Pia kuwalinda
wamiliki na watumiaji wa huduma hizi dhidi ya vitendo vinavyoweza kupelekea
kupoteza fedha na mali zao, pamoja na kuzuia watu binafsi, taasisi na vikundi
vya kijamii kutumika kufanya uhalifu ikiwemo utakasishaji fedha haramu.
2.
Benki Kuu
inafahamu kuwa baadhi ya watu binafsi, taasisi na vikundi vinavyotoa huduma
ndogo za fedha vikiwemo VICOBA, havina usajili rasmi na hivyo havitambuliki
kisheria. Kwa kutambua hilo, Sheria imeweka kipindi cha mpito cha mwaka
mmoja (kuanzia sheria itakapoanza kutumika rasmi) kwa wote wanaojihusisha na
utoaji huduma ndogo za fedha, kujipanga ili wawe tayari kusimamiwa pale kanuni
zitakapokuwa zimetolewa rasmi. Hivyo, katika kipindi hiki cha mpito, siyo kosa
kwa watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutokuwa na usajili rasmi.
Aidha, Wadau wote watashirikishwa kikamilifu katika utayarishaji wa
Kanuni hizo, na mara zitakapokuwa tayari na kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania,
maelezo zaidi kuhusu usajili yatatolewa.
Benki
Kuu inawasihi wananchi wote kutokuwa na taharuki na inasisitiza kwamba uamuzi
wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha umechukuliwa kwa nia njema na
kwa faida ya watumiaji na watoaji wa huduma hizi.
Aidha,
Benki Kuu inautahadharisha umma kujiepusha na taarifa na miongozo
inayotolewa kiholela na watu, kampuni na mashirika ambayo yanajitangaza kufanya
shughuli za uandikishaji wa watoa huduma ndogo za fedha kwa wananchi kwa niaba
ya Serikali au Benki Kuu.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu,
kampuni au shirika lolote litakalojihusisha na vitendo vya kuwakanganya
wananchi kwa lengo la kupotosha au/na kujipatia mapato haramu.
Tunawahamasisha
wananchi kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tangazo hili zinazoendelea kutolewa na
Benki Kuu katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu usimamizi wa watoa huduma
ndogo za fedha Tanzania Bara.
Kwa ufafanuzi/maelezo
zaidi wasiliana nasi kwa simu 022-2235585/0767503145 au barua pepe:
au tembelea Benki Kuu Makao Makuu Mtaa wa 2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam
Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha.
No comments:
Post a Comment