Tuesday, January 15, 2019

MGALU ACHANGIA MIL. 43 KATIKA SHUGHULI ZA KIJAMII NA KIMAENDELEO PWANI

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

MBUNGE wa viti maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu, amechangia shughuli za maendeleo katika wilaya mbalimbali mkoani hapo, iliyogharimu sh. milioni 43 kwa kipindi cha mwaka mmoja.


Aidha amekabidhi vifaa vya ofisi vyenye thamani ya milioni 5, kwa ofisi za jumuiya ya UWT katika kata zote 133 kimkoa ili kurahisisha utendaji kazi na kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.


Akitolea ufafanuzi juu ya utekelezaji wa shughuli zake za kibunge wakati wa baraza la UWT mkoa, Subira alisema moja ya majukumu yake ni kuunga mkono juhudi za serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kushiriki shughuli za kijamii.


Alisema kati ya mambo alitoshiriki kuweka mkono wake ni pamoja na kujitolea mifuko ya saruji kwenye ujenzi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.


Hata hivyo Subira alieleza, katika kutekeleza ilani kwenye sekta ya nishati alianzisha kampeni ya zima vibatari ,washa taa kwa kuchangia taa za solar akiambatana na uongozi wa UWT Mkoa wa Pwani .


“Taa hizo nilizigawa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu hususan katika mashule kwa lengo la kuboresha elimu bora kwa wanafunzi na zahanati kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa huduma za kiafya ikiwemo wadi za kujifungulia, uboreshaji wa afya za mama wajawazito ,watoto na kurahisisha huduma za afya kwa makundi maalum”. 


“Pia niliambatana na mrs. Barbara Wentworth wa Wentworth Foundation na kutembelea shule ya sekondari Mandela na kukabidhi vitaulo yaani PADS kwaajili ya wanafunzi wa kike;”alifafanua Subira.


Subira alibainisha, taulo hizo ni za mwaka mzima kwa kila msichana, kwa wasichana 500, huo ni msaada mkubwa na utasaidia kuboresha mahudhurio yao darasani ,amekabidhi maboksi ya vitabu na kuahidi kujenga maktaba.


Mbunge huyo, ambae pia ni naibu waziri wa nishati alisema kwamba, licha ya majukumu hayo amefanya ziara wilaya mbalimbali kukagua miradi ya ujenzi wa nishati ya umeme na kuwasha umeme katika maeneo mbalimbali ya mkoa .


Anaipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais dkt.John Magufuli kwa jitihada za kuondoa changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye baadhi ya maeneo.

No comments:

Post a Comment