Thursday, January 17, 2019

MIL. 40 ZAKARABATI MABWENI CHANGARIKWA, CHALINZE.


Mwenyekiti wa Bodi ya shule Sekondari ya Changalikwa Omari Mhando akikagua moja ya mabweni yanayokarabatiwa.
Picha na Omary Mngindo.
...........................................................


Na Omary Mngindo, Chalinze.

KIASI cha shilingi milioni 40 zilizotolewa na Halmashauri ya Chalinze, wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, zinakarabati mabweni manne katika shule ya sekondari ya Changarikwa iliyoko Kata ya Mbwewe wilayani hapa.


Hatua hiyo inalenga kuboreshwa kwa miundombinu shuleni hapo kwenye mabweni ya Benjamen Mkapa, Jakaya Kikwete na Salma Kikwete, ili wanafunzi wawe katika mahali safi na salama wakati wakipata elimu yao.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi shuleni hapo Omary Mhando, aliyewahi kuwa diwani kwenye Kata hiyo miaka kadhaa iliyopita, ambapo alisema wamepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 40 kwa ajili ya zoezi hilo.


Aliongeza kwamba awali mabweni hayo yalikuwa katika hali mbaya kutokana na uchakavu wa milango na madirisha, ambapo baada ya kupatikana kwa fedha hizo kazi inakwenda vizuri, na kwamba wanategemea kumalizika ifikapo mwishoni mwa mwezi wa pili.


"Shule yetu chini ya Mwalimu Mkuu
Sylivester Omari imekiwa na  changamoto kubwa ya uchakavu wa milango na madirisha, tukaomba fedha halmashauri yetu ya Chalinze, wakatuingizia kiasi cha shilingi milioni 40 ambazo tunaendelea nazo katika ukarabati," alisema Mhando.


Aliongeza kwamba mpaka sasa wakati kazi hiyo ikielekea ukingoni wametumia kiasi cha shilingi milioni 13, na kwamba wanataraji kutengeneza vitanda vya chuma vipatavyo 100 katika fedha hizohizo za shilingi milioni 40.


Kwa upande wake mwalimu Tete Emulike amezungumzia changamoto ya ukosefu wa uzio shuleni hapo, hali inayosababisha ufinyu wa usalama wa mali za shule, na wamafunzi na kwamba kipindi cha mapumziko ya wanafunzi kunakuweo na uvamizi mkubwa wa mifugo.


"Shule yetu ina eneo kubwa ambalo halina uzio, hali hii inahatarisha usalama wa wanafunzi na vifaa, pia kipindi cha likizo za wanafunzi mifugo inakuwa kero kwani inaingia ndani ya eneo hali inayosababisha usumbufu mkubwa," alisema Mwalimu Emulike.


Nae mmoja wa mafundi aliyejitambulisha kwa jina la Juma Semlamba alisema kwamba kazi ya ukarabati wa milango itakamilika ndani ya siku saba kuanzia Jumatano ya Jan 16 na kukabidhi kazi hiyo.


Ukarabati huo mbali ya milango ya mbao katika vyumba vya mabweni hayo, pia imewekwa milango ya vyuma (Mageti) nje ya mabweni hayo hali inayothibitisha kuimarishwa kwa miundombinu hiyo.

No comments:

Post a Comment