Tuesday, January 15, 2019

TFDA YAIMARISHA UDHIBITI WA BIDHAA KATIKA VITUO VYA FORODHA.

Mkaguzi wa dawa wa TFDA kituo cha Namanga akiendelea na ukaguzi.
......................................

NA WAMJW-ARUSHA

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kaskazini imeeleza kuwa, itaendelea kulinda soko la ndani la bidhaa za vyakula ,dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuimarisha huduma kwenye mipaka yote nchini ikiwemo mpaka wa Namanga, Mkoani Arusha.

Udhibiti katika mipaka hiyo ni unalenga kuhakikisha kuwa bidhaa bora, salama na zenye ufanisi pekee ndiyo zinaingia nchini ili kulinda afya ya wananchi.

Hayo yamebainishwa katika kituo cha TFDA kilichopo Mpaka wa Namanga mkoani hapa wakati wa Maafisa Uhusiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo walipotembelea Kituo hicho cha ukaguzi ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni ya ‘ Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.

Maafisa ukaguzi wa Mpaka wa Namanga ambao unatenganisha nchi za Tanzania na Kenya walieleza mikakati ya utoaji wa huduma za ukaguzi kutokana na Serikali kuwekeza rasimali watu pamoja vitendea kazi katika kurahisisha utoaji wa huduma katika Mpaka huo.

Kaimu Meneja TFDA Kanda ya Kaskazini, Benny John amesema ofisi ya Kanda imeendelea kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwemo udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa vipodozi, vifaa Tiba na vitendanishi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata kanuni na sheria zilizowekwa katika kuhakikisha wanalinda maslahi mapana ya kulinda afya ya wananchi.

“Udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini umeongezeka kwa wafanyabiashara kulipa ada na tozo za Serikali na hivyo kuongeza pato la Taifa” alisema Kaimu Meneja huyo.

Nae Mkaguzi wa Dawa wa TFDA Mpaka wa Namanga, Bw. Elia Nyeura amesema takwimu za uingizaji wa mizigo katika kituo cha Namanga zimeongezeka kutoka shehena 724 mwaka 2015/16 hadi kufikia 1,223 kwa mwaka 2016/2018.

“Kwa sera ya awamu ya tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda, bidhaa zinazodhibitiwa na TFDA na kuruhusiwa kwenda nje ya nchi hususani zilizosindikwa kwa kipindi cha miaka mitatu zimeongezeka kutoka shehena 429 hadi kufikia 640 kwa 2017/18 ” amesema Nyeura na kuongeza kuwa, mamlaka imepunguza upotevu wa mapato kutokana na bidhaa zisizofaa kwa kuimarisha ukaguzi”. Alisema.

Hata hivyo amebainisha kuwa thamani ya bidhaa zilizokamatwa kwa kuingizwa nchini bila kufuata utaratibu zimepungua kutoka Milioni 630.3 hadi kufikia Milioni 24.7 kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018.

Aidha, maafisa Uhusiano hao wameweza kutembelea maeneo mbalimbali ya kituo hicho ikiwemo chumba maalum cha Maabara na kujionea namna bidhaa za dawa zinavyochunguzwa katika kuangalia ubora wake kabla hazijaingizwa Nchini.

Mpaka wa Namanga ni moja ya mipaka ambayo tayari imeanza kufanya kazi kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa kwa upande mmoja tu wa Nchi (One Stop Boder Post-OSBP) ambapo bidhaa inaingia na kukaguliwa kwa pamoja na wakaguzi wa nchi mbili (Tanzania na Kenya) ili kupunguza muda wa wadau kukaa mpakani kwa muda mrefu kwa ukaguzi.

No comments:

Post a Comment