Friday, January 18, 2019

WASTAAFU DAWASA WAMPONGEZA MAGUFULI

Na Omary Mngindo, Mlandizi

WASTAAFU wa Shirika la Maji (DAWASA) Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, wamempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kusikiliza kilio cha Wastaafu, huku wakimuomba atupie jicho shirika hilo, ili wapate mafao yao stahiki.

Wakizungumza na Waandishi wa habari, baadhi ya Wastaafu hao kwa niaba ya wenzao walianza kupongeza Rais Magufuli, huku wakiomba kuangaliwa Mkataba wao wa hali bora kazini ambao viongozi wao waligoma kuusaini.

"Kiukweli Rais John Magufuli ameonesha ni kiongozi bora anayejali maslahi ya wananchi, nasi Wastaafu tuliolitumikia Shirika la Maji Dar es Salaam (DAWASA) tunamuomba atupie jicho, tunadai Mkataba wa hali bora kazini, viongozi waligoma kuusaini," alisema Suleiman Sule.

Nae Elidrick Chichwa akizungumza kwa niaba ya wenzake ambao hawakupenda kutaja majina yao, alisema kuwa wanamuomba Waziri wa Maji awasaidie wapate haki yao ya mafao ya kustaafu kupitia Mkataba huo.

"Tunaimani kubwa na Serikali iliyopo Madarakani inayojali wanyonge, kupitia Waandishi wa Habari tunaimani kwamba kilio au ombi letu litapokelewa na viongozi husika, kisha kufanyiwakazi," alisema Chichwa.

Mstaafu mwingine alisema kwamba yeye alifanyakazi Shirika la Maji Dar es Salaam (DAWASA), City Water na DAWASCO na kwamba wakati wakiwa kazini kuna Mkataba wao wa hali bora ambao uliandikwa ambao hata hivyo haukusainiwa na viongozi wao.

"Nimefanyakazi kwa miaka 26, cha kishangaza nimestaafu mwezi wa nane mwaka 2018 nikaambulia sh. Mil. 11 tu, kama Mkataba wa hali bora kazini ningepokea kiasi cha sh. Mil. 80, kwa sasa naishi maisha magumu sana," alisema Mstaafu huyo.

Wamemalizia kwa kumuomba Waziri mwenye dhamana wa Wizara hiyo kuangalia mkataba huo, ili wastaafu hao nao wanufaike na miaka waliyosaidia ujenzi wa nchi kwa kipindi chote.


No comments:

Post a Comment