Thursday, January 3, 2019

DC BAGAMOYO ATAKA KASI YA KUKUSANYA MAPATO IONGEZEKE.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, akizungumza na katika kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya (DCC).
................................. 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, amewataka wahasibu wa Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo, kuacha kukaa ofisini muda mrefu na badala yake wafike kwenye vyanzo vya mapato ili kujionea hali halisi ya mapato halisi katika maeneo husika.

Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.

Amesema kazi ya kukusanya fedha inahitaji ufuatiliaji hivyo ni wajibu wa wakuu wa idara kuhakikisha mnafuatilia walipa ushuru kwenye vyanzo ili kujiridhisha endapo malipo wanayolipa yanalingana na kile walichobeba au kuzalisha.

Amesisitiza swala kuongeza mapato ndani Halmashauri zote mbili kwakuwa fedha hizo zinaweza kutatua baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa.

Awali Afisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao, akisoma taarifa ya utendaji kazi shughuli za Halmashauri hiyo, alisema mapato yameendelea kukua mwezi hadi mwezi na kufikia milioni 600, kwa mwezi wa Oktoba na Novemba 2018 kutoka milioni 400 mwezi Julai 2018.

Milao alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Mkuu wa wilaya kufuatilia kwa karibu vyanzo vya mapato na namna watumishi wa Halmashauri wanavyokusanya hali iliyoleta msukumo na kuongezeka kwa mapato.

Aidha, Milao alitaja changamoto zinazowakabili katika kufikia lengo ikiwa ni pamoja uelewa mdogo wa wafanya biashara juu ya ulipaji kodi ya huduma za mji pamoja na uhaba wa vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, Afisa mipango huyo amesema Halmashauri imejiwekea mikakati ya kuhakikisha inaendelea kuwahamasisha wananchi juu ya umuihmu wa kulipa kodi ya huduma na kuwachukulia hatua wale wote wenye madeni sugu.

Katika hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ameonyesha kutoridhishwa na mapato hayo na kutaka kasi iongezwe katika ukusanyaji ili kufikia milioni mia tisa kutoka mia sita za sasa.

Alisema tayari ameshafanya uchunguzi na kubaini fedha nyingi zinazopotelea kwenye mifuko ya watu na kwamba hatokubali mapato ya Halmashauri yapotee.

Aliwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Chalinze na Bagamoyo kuhakikisha wanasimamia ukusnyaji wa mapato na kwamba ikitokea mkuu wa idara husika anazembea katika kufuatilia na kukusnaya mapato atahakikisha anamuwajibisha.
 
 Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya ya Bagamoyo wakiendelea na kikao. 


 Afisa Mipango Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).
 
Afisa Mipango Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard M. Kapinga akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).

No comments:

Post a Comment