Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa mamlaka ya maji
Lindi Mhandisi Adam Alexanda aliyeshikilia makabrasha
kutokana na kushindwa kusimamimia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika
manispaa ya Lindi pamoja na matumizi mabaya ya ofisi, Waziri mkuu
amemuelekeza Mkuu wa Kupambana na rushwa TAKUKURU mkoani Lindi kufanya
uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mhandisi huyo.
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander akisikiliza maagizo
ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
.......................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya
ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika
Manispaa ya Lindi.
Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa
Lindi, Bw. Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala
hilo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 19, 2016) wakati
alipotembelea mradi wa maji wa Ng’apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na
Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.
“Kamanda wa TAKUKURU fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema
analipwa Wizarani, mimi najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda
kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” amesisitiza Waziri
Mkuu.
Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya
fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya
mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda
mrefu.
Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata
shida huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo
vyao vya kazi. “Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam.”
Alipoulizwa sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi
huyo alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili
ya kutatulia changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.
“Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na
unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu!
Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa sh.150,000. Hatuwezi
kuvumilia hali hii,” amesema.
No comments:
Post a Comment