Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa
Ummy A. Mwalimu anapenda kutoa ufafanuzi kuhusu Tamko la Shirikisho
la Watu Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kuhusu makundi ya wananchi
wanaostahili kupata msamaha wa matibabu.
Aidha, baadhi ya Vyombo vya habari vimenukuu maelezo ambayo
yametolewa na mwenyekiti wa SHIVYAWATA kuhusu Makundi yanayostahili
kupata msamaha wa Matibabu nchini.
Kutokana na Maelezo hayo, napenda kutoa ufafanuzi ufuatao; Sera ya
Afya ya Mwaka (2007) inatambua kuwa wapo wananchi ambao wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali katika kuzifikia huduma za Afya wakiwemo watu
Wenye Ulemavu.
Aidha, Kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9/2010 ambayo, pamoja na
mambo mengine, Sheria inabainisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wana haki ya
kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za Afya.
Kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Afya (2007) na Sheria ya Watu Wenye
Ulemavu(2010) Wizara yangu inatambua na itaendelea kuhakikisha kwamba
Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kugharamia huduma za Matibabu
wanapatiwa Msamaha wa Matibabu katika Ngazi zote kuanzia Zahanati, Vituo vya
Afya, Hospitali za Mikoa na Hosptali za Rufaa.
Pia kwa kutambua umuhimu wa huduma ya Afya kwa Wananchi wote, Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika
mchakato wa kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo Watu
Wenye Ulemavu kupata Kitambulisho cha Bima ya Afya.
Hatua hii itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu Wenye Ulemavu
katika kuzifikia huduma za Afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.
Naomba kuchukua fursa hii kuwahakikishia ndugu zangu Wenye Ulemavu kuwa
wanayo haki ya kupata huduma za matibabu katika ngazi zote.
Aidha, Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha makundi
maalum wakiwemo watu Wenye Ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma
za Matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika vituo vyote vya
kutolea huduma za afya.
Natoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwatambua Watu
Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha
Kitengo cha Huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya kutolea huduma za
Afya ili viweze kuwatambua na kutoa msamaha kwa watu wenye ulemavu wasio
na uwezo ili waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu wa fedha.
Aidha, ni marufuku kwa Mtumishi yeyote wa Sekta ya Afya kuonesha
vitendo vyovyote vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu Wenye Ulemavu wanaofika
katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mtumishi atayethibitika kuonesha
kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za Afya kwa kufanya
vitendo vya vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maaalum ikiwemo
watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa
kazi.
Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Vile vile, ninawataka watoa huduma wote kuwapa kipaumbele watu wenye
ulemavu wanapofika hospitali. Wapatiwe huduma haraka ili kuwapunguzia
usumbufu kutokana na mahitaji yao ya kimwili.
Kama ambavyo tumefanya kwa Wazee niwaagiza kila kiongozi ahakikishe
anaweka utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya kwanza watu wenye ulemavu
tukijifunza kwa jinsi tulivyofanya na kufanikiwa katika eneo la kuhudumia
wazee.
Watu wenye ulemavu ni wenzetu, watoto wetu, ndugu na jamaa zetu.
Tuwahudumie kwa upendo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine.
Imetolewa na
MHE. UMMY A. MWALIMU (Mb.)
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto.
15/10/2016
No comments:
Post a Comment