Diwani
wa kata ya Vigwaza Muhsin Baruan akimkabidhi dawa alizotoa msaada kuungana
mkono juhudi za serikali kutatua changamoto za uhaba wa dawa ,mganga
mfawidhi wa zahanati ya Ruvu darajani ,Dkt. Gilbert Mkotigwa.
Diwani
wa kata ya Vigwaza Muhsin Baruan akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada
wa dawa mbalimbali katika zahanati ya Ruvu darajani na Vigwaza yenye
thamani ya mil.4.5
...........................
DIWANI wa kata ya Vigwaza ,Halmashauri ya Chalinze
mkoani Pwani, Muhsin Baruan ametoa msaada wa dawa za magonjwa mbalimbali katika
zahanati mbili ya Vigwaza na Ruvu Darajani, zenye thamani ya mil.4.5.
Diwani huyo ametoa dawa hizo ili kukabiliana na
changamoto ya upungufu wa dawa inazozikabili zahanati hizo ambapolengo ni
kutatua changamoto hizo.
Aidha pamoja na
msaada huo, Baruan ametoa matofali 1,000 pamoja na mifuko ya saruji 30
kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba ya mganga mfawidhi wa zahanati ya Ruvu
Darajani.
Akikabidhi misaada hiyo ,katika zahanati
hizo,alisema ataendelea kutatua matatizo yanayowakabili wakazi wa kata ya
Vigwaza katika hudumambalimbali za kijamii, zikiwemo afya, maji, elimu pamoja
na kusaidia makundi maalum ikiwemo vijana, walemavu, wanawake na wazee ili
aweze kutimiza lengo la kuchaguliwa kwake na kutekeleza yale ambayo aliwaahidi wananchi
wake.
Alisema fedha zilizotumika kununulia dawa hizo, mifuko
ya saruji na matofali ni nguvu yake mwenyewe na ni moja ya ahadi zake
alizoahidi kuzitatua ambapo umefika wakati sasa wakutimiza.
Aliongeza kuwa kwasasa watumishi wa afya katika
zahanati hiyo wanaishi katika nyumba za kupanga na kupata kero hasa nyakati za
usiku akitokea mgonjwa wa dharura.
Kufuatia hali hiyo aliwaomba wadau wa maendeleo, ya afya wajitokeze kushirikiana kujenga nyumba hiyo ili kuondoa kero ya kuishi mbali ya kituo hali inayopelekea madhara kwa wagonjwa na usumbufu kwa mganga.
Baruan aliishukuru serikali kwa kuingiza zahanati ya
Ruvu Darajani na kuiomba ipeleke dawa kwenye zahanati kwa wakati ili kuwaondolea
usumbufu wananchi.
Aidha,
alitumia nafasi hiyo kumtaka mganga mfawidhi katika zahanati ya Ruvu Darajani, afisa
mtabibu zahanati ya Vigwaza, kuzitunza dawa hizo na kuzitumia pale inapostahiki kwa uadilifu.
Kwa upande wake, mganga mfawidhi wa zahanati ya Ruvu
Darajani, Gilbert Mkotigwa, alisema zahanati hiyo ilikuwa haijaingizwa katika
mgao wa dawa kutoka bohari ya madawa (MSD) kwa miaka mitatu iliyopita tangu feb
2014 hadi sept 5 mwaka huu.
Alisema katika kipindi hicho walikuwa
wakisaidiwa na zahanati za jirani ikiwemo Visezi, Kidogozero, Milo, Vigwaza
pamoja na wilaya ambayo ilikuwa ikitoa mgao kutokana na fedha za OC.
Dk,Mkotigwa alisema kutokana na uhaba huo wa dawa,
Diwani aliomba orodha ya dawa zinazohitajika na kufanikiwa kuziwasilisha.
Alisema licha ya kupokea msaada huo lakini bado zahanati inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa nyumba ya mganga na watumishi wengine, wodi ya uzazi ambapo kwa sasa kina mama wanajifungulia katika chumba kidogo sana, mashine za kupimia wingi wa damu, sukari na haja kubwa.
Dk.Mkotigwa alisema kukosekana kwa mashine ya
kupimia wingi wa damu kunasababisha wajawazito kwenda kupima wingi wa damu
kituo cha afya Mlandizi ambayo imekuwa kero kwa wajawazito kufuata huduma hiyo
mbali huku ikiwa ni kipimo muhimu kwao tangu kushika mimba hadi kujifungua.
Alimuomba diwani huyo kushirikiana na wahisani
wengine kuangalia namna ya kusaidia upatikanaji wa vipimo hivyo na kutafutia
ufumbuzi changamoto hizo ili kutoa huduma bora.
Alisema zahanati hiyo inahudumia wagonjwa katiya 400-500
kwa mwezi na wajawazito 10 hadi 15 katika kipindi hicho.
Afisa tabibu wa zahanati ya Vigwaza ,Alexander Ngalawa ,alisema zahanati hiyo ina hudumia vijiji vitano na ipo karibu na barabara kuu ya Morogoro-Dar-es salaam hivyo watu wengi kukimbilia kupata huduma ya afya.
Alisema bado wana upungufu wa madawa ,unaotokana na
kupelekewa upungufu wa madawa wanayooda kupitia wilaya kwenda bohari na kusababisha
upungufu katika mahitaji yao.
Dk.Ngalawa alieleza kwenye zahanati hiyo wapo
watumishi watatu ambao hawatoshi ,mmoja akipata likizo wanabaki wawili ambao
wanazidiwa na wagonjwa.
No comments:
Post a Comment