Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii,
Peter Serukamba amesema kuwa uanzishwaji wa Mfuko wa Mafunzo ya Habari
utaweka utaratibu wa maslahi ya waandishi wa habari utakaowasaidia kuwa na bima
za afya, mikataba inayoeleweka pamoja na kuwaendeleza kimasomo.
Serukamba aliyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akihitimisha
kikao cha Kamati hiyo kilichokuwa kikijadili juu ya muswada wa habari ambao kwa
mara ya kwanza uliwasilishwa Bungeni mnamo mwezi Septemba mwaka huu.
Serukamba amesema kuwa Kamati hiyo imesikiliza maoni ya kila mmoja na
imejitahidi kupitia kifungu hadi kifungu cha muswada huo na Serikali imekubali
kuyafanyia mabadiliko baadhi ya maeneo ya muswada huo kulingana na maoni
yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali.
“Muswada huu utakapokuwa sheria tunategemea kuunda Mfuko wa Mafunzo wa
Habari ambao utawaendeleza waandishi wa habari kwa kuwawekea utaratibu wa
maslahi yao, utakuwa ni kwa ajili ya waandishi wa habari wote
watakaothibitishwa na Bodi ya Ithibati”, alisema Serukamba.
Amefafanua kuwa mfuko huo utawezesha mafunzo kwa wanataaluma ya habari,
utakuza programu za uendelezaji maudhui ya ndani ya nchi pamoja na kuchangia
utafiti wa maendeleo katika nyanja za habari na mawasiliano ya umma, hivyo,
utasaidia kurudisha taaluma ya habari kwenye hali nzuri nchini.
Aidha, ameongeza kuwa sheria hiyo itahakikisha inalinda haki za waandishi
wa habari, vyombo vya habari pamoja na wananchi wa kawaida kwa sababu
itaweka utaratibu juu ya utatuaji wa kesi zinazohusiana na vyombo
vya habari kwa muda mfupi hivyo kusaidia watu kupata haki zao haraka.
Muswada huo pia umetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa wanahabari
kujiendeleza kielimu katika taaluma ya habari ili wawe na vigezo
vitakavyowawezesha kuwa wanahabari kamili waliobobea kwenye taaluma hiyo.
No comments:
Post a Comment