Sunday, October 30, 2016

DC BAGAMOYO AAHIDI KUZISIMAMIA ASILIMIA 10 YA FEDHA KUTOKA HALMASHAURI ZIWAFIKIE VIJANA NA KINAMAMA.

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Majidi Mwanga amesema kuwa atahakikisha anazisimamia ipasavyo fedha  amabazo zinazotolewa na Halmashauri kwa ajili ya  kuwasadia vijana na kinamama lengo ikiwa ni kuona zinatumika katika vikundi mbalimbali lli kukuza uchumi na kuleta chachu ya kimaendeleo.

Mwanga ameyasema hayo jana wakati alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio cha Jijini Dar es Salaam kuhusiana na changamoto  mbali mbali zilizopo katika utendaji wa kazi pamoja na mikakati aliyoiweka katika kuwahudumia wananchi wake wa Bagamoyo.

Alisema kwamba halmashauri zinanapaswa kutenga kiasi cha asilimia kumi cha makusanyo ya mapato yake ambapo vijana wanatakiwa kupatiwa asilimia tano na kwa upande wa kinamama wanatakiwa wapatiwe asilimia tano kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za ujasiriamali.

“Mimi kama mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mikakati yangu ni kuhakikisha kwamba fedha hizo ambazo ni asilimia kumi zinawafikia walengwa wote bila ya kuwa na ubaguzi, hivyo nitazisimamia na kuona ni jinsi gani zinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa vijana pamoja na kinamama ambao watapatiwa fedha hizo,”alisema Mwanga.

Aidha mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba ana imani kwamba endapo Halmashauri ikitilia mkazo suala hilo la kuhakikisha  asilimia kumi inatolewa katika kila bajeti kutaweza kuwa mkombozi mkubwa kwa kuviwezesha vikundi vya aina mbali mbali ili viweze kuendesha biashara zao na kukuza mitaji waliyonayo.

Pia alifafanua kuwa fedha hizo zinatolewa kwa utaratibu maalumu ambapo inatakiwa vijana au kinamama kuunda vikundi vyao na kuvisajili ili pindi fedha hizo zinapotolewa ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati na  kuwanufaisha kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza biashara zao ambazo  wanazifanya ili kukua zaidi.

 “Katika Wilaya yangu ya Bagamoyo kwa sasa nina halmashauri mbili, ambapo kuna halshauri ya Bagamoyo, pamoja na halmashauri ya mji mdogo Chalinze, kwa hivyo zote hizi zinatakiwa kutenga asilimi hiyo kumi kwa ajili ya  vikundi hivyo ” aliongeza Mwanga.

Alisema kwamba kwa sasa kuna fedha ambazo tayari zimeshatolewa na halmashauri  kwa ajili ya kuvisaidia vikundi hivyo vya kinamama na vijana, ambapo katika halmashauri ya bagamoyo kumeshatolewa kiasi cha shilingi milioni 120 na kuongeza kuwa fedha hizo zitakuwa zinatolewa kwa mzunguko ili ziweze kuwafikia walengwa wote.

Katika hatua nyingine Mwanga alitoa wito kwa vijana na wakinamama ambao watapata fursa ya kupatiwa fedha hizo kuhakikisha   wanazitumia vizuri katika kuendeshea biashara zao ili kukuza waweze kuirejesha kwa wakati na vikundi vingine vipatiwe pia.

1 comment:

  1. Tatizo vikundi vyetu (vyote Vya vijana na akina Mama), uongozi ukiwekwa, wanadamu kuwa ni ajira na kukazia maatumizi mbadala ya uzalishaji. Lazima Mkuu uwabadilishe fikra. La sivyo hata yakiwekwa mamilioni yatadidimia tu bila kuleta tija.

    ReplyDelete