Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika Louis Rene Peter Larose (hayupo
Pichani), makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington DC, Marekani, kulia kwake
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James.
........................................
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali
imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango
mkubwa kuinua uchumi wa Taifa pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika
lindi la umasikini.
Waziri Mpango ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani,
wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia
Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia
masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi
hiyo.
Amesema kuwa kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo
mapinduzi yanayokusudiwa katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa
kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya wakulima.
Kuhusu sekta ya Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa
wataalamu wa Uchumi na Fedha katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya
Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia
kupitia upya kodi zinazoleta kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.
Eneo jingine alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia
Tanzania Mkopo na ruzuku utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa
inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa
Umeme nchini, TANESCO, ili shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na
kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa haraka.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia
Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja
na miradi mingine, itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini
“Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya
kilimo kuwa na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Mimi nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama
kuzidi hadhi ya Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo
zikisimamiwa vizuri zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.
Ameitaka Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha
malengo yake ya maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba
anaongoza kundi la nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania
kama zilivyo nchi nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais
Dkt. John Pombe Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na
ametoa pole kwa nchi hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko
kubwa la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.
Ameahidi kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti
na kuishauri nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya
matetemeko pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa
majanga kama hayo.
No comments:
Post a Comment