MADEREVA wa matipa ya mchanga ,wanaotumia barabara kuu ya Dar es salaam
–Morogoro, wamefanya mgomo baridi ,kulalamikia wakala wa barabara
(TANROADS)mkoani Pwani,unaowakamata kutokana na kutofunga mchanga vizuri na
kuwapiga faini ya sh.500,000.
Madereva hao waliweka mgomo huo katika eneo la Tamco ambapo ndipo
watendaji wa wakala huo walikuwa wakiwasimamisha kwa ajili ya kukagua wale
waliojaza mchanga hali inayosababisha kuchafua miundombinu ya barabara.
Dereva Martine Magari na Emmanuel Shao,walisema ni kweli wapo madereva
wasiofunga vizuri maturubai ya magari yao lakini tatizo kubwa ni kukosa elimu
ya kufunga kwa ubora.
Shao aliziomba idara ama mamlaka husika kutoa elimu juu ya sheria
mbalimbali kwani inakuwa sio rahisi kuelewa sheria zote zinazotungwa bila
kupatiwa elimu ya kutosha.
“Unaona fuso dogo kama lile,huwezi amini ni sh.500,000 kikweli ni kubwa
,sasa unakuta tunalalamika kutokana na kwamba hatujui lolote kuhusu sheria zao”
“Halafu hatujafundishwa kufunga hooks wanavyotaka wao wakala wa
barabara,kila mtu anaufungaji wake lakini endapo watatuelewesha vizuri haina
shida.
“Sasa wao wanapanda juu ya gari na kuchokonoa chokono matokeo yake
ndio inakuwa shida ,mchanga unamwagika”alisema Shao.
Magari aliutaka wakala huo kukagua kwa macho na sio kupekenyua maturubai
kwa kuingiza mikono kwani kwa kufanya hivyo ni lazima mchanga mwagike.
“Madereva pia wamekasirika kwa hilo huwezi kukagua hadi uingize mikono
,kwakuwa mikono inasababisha mchanga kumwagika halafu unatozwa hela yote
hiyo”alifafanua Magari.
Kwa mujibu wa kaimu meneja TANROADS mkoani Pwani,injinia Yudas
Msangi,alisema wapo kwenye operesheni ya kukagua magari ,kwa kufuata sheria ya
barabara ya mwaka 2007 namba 13 kifungu namba 46C, inayokataza kuchafua
barabara.
Alieleza kuwa hakuna anaewaonea madereva hao ,kwani wanatambua vilivyo
kuhusu sheria hiyo na mara kwa mara huwa wakielimishwa kuacha tabia ya kuzembea
kufunga mchanga vizuri.
Injinia Msangi alisema,wanatoa muda hadi jumatatu ijayo zoezi hilo
litaendelea ili kudhibiti uchafuzi huo wa miundombinu ya barabara.
Alisema wanatakiwa wasijaze mchanga kwakuwa unaathiri matairi ya magari
mengine yanayopita,kusababisha ajali ,kufukia mifereji na kufuta alama za
barabarani na hatimae kuipa mzigo wakala huo.
Injinia Msangi alisema lengo ni kuacha kumwagwa mchanga na kufunga matipa
ya mchanga kwa ubora ili kuepusha matatizo na kuiondolea hasara TANROADS.
Aliwataka madereva wa matipa ya mchanga kuacha kudharau sheria zilizopo
ili kuepuka migongano isiyo na tija.
Awali kamanda wa usalama barabarani,Abdi Issango ,alifika eneo la tukio
na kuzungumza na madereva hao ,uongozi wa tanroads mkoa,akiwemo kaimu
meneja,msaidizi wake pamoja na meneja wa barabara mkoa mama Urio.
Alisema ni kweli madereva wengi wamekuwa hawafungi vizuri mchanga kwa
kutumia kifungio(hooks)kwenye maturubai ili kuzuia mchanga usimwagike.
Hata hivyo kamanda Issango,alisema kwa kushirikiana na wakala wa barabara
mkoani humo,wameamua kutoa muda ili kurekebisha mapungufu yaliyopo ambapo
kuanzia jumatatu atakaekiuka maelekezo yaliyotolewa atalipa faini ya
sh.500,000.
Akizungumzia kiwango cha faini kinacholalamikiwa,alieleza kila idara ina
sheria zake, kwa usalama barabara ukikiuka sheria adhabu yake ni sh.30,000
lakini kwa Tanroads ni 500,000 na kutoingia kwenye mizani faini zake huwa
ni mil.2 .
Baada ya kamanda huyo kuzungumza na pande hizo mbili ,madereva hao
walitawanyika na kuridhia maelekezo waliyopatiwa sambamba na kukubaliana kuanza
kwa zoezi hilo wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment