Bodi ya Filamu Tanzania leo imemkabidhi cheti na hundi yenye thamani ya
shilingi Laki Mbili mwanafunzi Omary Maganga aliyefanya vizuri kwenye masomo ya
filamu na runinga kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA).
Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ofisi za
bodi hiyo ambapo Afisa Uhusiano na Mawasiliano Abuu Kimario alimkabidhi cheti
hicho na hundi kwa niaba ya Katibu Mtendaji Joyce fisoo.
Baada ya kukabidhiwa zawadi zake bwana Maganga
aliishukuru Bodi hiyo ya filamu kwa kutambua juhudi za wanafunzi wanaofanya vizuri
kwenye masomo yao. Pia ameziasa taasisi zingine za Serikali na zisizo za
kiserikali kuwatambua wanafunzi wanaofanya vizuri kwani kwa kufanya hivyo
kunaongeza morali na ushindani.
Wakati huo Afisa Uhusiano na Mawasiliano Abuu
Kimario kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa bodi hiyo ametoa ahadi ya kuendelea
kutoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo yenye uhusiano na
tasnia ya filamu.
Kwa sasa Bodi ya Filamu Tanzania iko kwenye utekelezaji wa programu ya
kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya
tasnia ya filamu nchini. Program hii ilianzishwa ikiwa na lengo la kukuza ubora
wa filamu za Kitanzania.
No comments:
Post a Comment