Mkazi
wa Kilindi, Tanga Angela Basso , aliyetembea kwa miguu kwa muda wa siku
21 pamoja na Watoto wake Janeth Peter (9) na Happy Peter (7) kuja
Mkoani Dodoma kuonana na Waziri mkuu ili kupeleka malalamiko yake ya
kudhulumiwa mashamba yake ya hekari 30 na kuchomewa nyumba.
.........................................
MKAZI wa Kilindi mkoani Tanga, Angela Basso, akiwa na watoto wake
wawili Happy(7) na Janeth Peter(9), amelazimika kutembea kwa miguu kwa siku 21
hadi mkoani Dodoma kwa lengo la kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili amsaidie
kurudishiwa hekari 30 za mashamba yake aliyozoporwa.
Basso alifika mjini Dodoma akiwa na watoto wake hao, ambapo alisema
aliona ni vyema kwenda Dodoma kuonana na Waziri Mkuu kutokana na kuporwa
mashamba na kuchomewa nyumba yake katika kijiji cha Kwendigole wilayani Kilindi
na wanaume wawili ambao waliojitokeza kwa nyakati tofauti wakidai ni maeneo
yao.
Alisema alipita hatua zote zinazotakiwa kuomba mashamba, ambapo awali
alipatiwa hekari 10 na kijiji na akazifanyia shughuli za kilimo na
kujenga nyumba yake ya kuishi, lakini baada ya kwenda kujifungua alikuta mazao
yamefyekwa na yeye kutakiwa kuondoka kwenye eneo hilo.
Mwanamke huyo alisema baada ya kunyang’anywa alifikisha malalamiko yake
kuanzia uongozi wa kijiji hadi wilayani na baadaye akapatiwa eneo jingine la
hekari 20, lakini alijitokeza mtu mwingine na kudai eneo hilo ni mali ya
kanisa, licha ya kumiliki kihalali eneo la Hembekali.
“Nilikwenda kushtaki kwa serikali ya kijiji, kata na baadaye kwenda kwa
mkuu wa wilaya ambako iliamuliwa nirudishiwe mashamba yangu, lakini hawakufanya
hivyo mwisho wa siku nikafukuzwa kabisa kuishi kwenye eneo hilo,” alisema Basso.
Mwanamke huyo alisema baada ya kutimuliwa alianza kuishi maisha yake
kituo cha mabasi Muheza na baadaye alifukuzwa kituoni hapo kwa madai watu
hawaruhusu kulala ama kuishi hapo na ndipo akaamua kuanza safari ya Dodoma
baada ya kusikia Waziri Mkuu amehamia Dodoma.
Akisimulia machungu ya safari yake, Basso alisema akiwa njiani walikuwa
wakila mahindi ya kukaanga na maji ya kunywa na kulala porini muda mwingine
giza linapowakuta katikati ya pori.
“Naomba kusaidiwa jamani nimeanza kufuatilia tangu mwaka 2012 lakini bila mafanikio jambo ambalo limechangia familia yake kusambaratika kutokana na kukosa pa kuishi huku watoto wangu hawa wakikosa elimu kwa kutangatanga,”alisema Mwanamke huyo.
Basso aliomba Serikali itende haki ili yeye aweze kupata haki yake ya
kurejeshewa mashamba yake na kurudi katika eneo hilo ili watoto wake wawili
wapate nafasi ya kusoma.
Mwanamke huyo alisema kwa sasa amekuwa kama mkimbizi kutokana na kukosa
hana mahali pa kuishi huku mumewe naye akiikimbia familia yake baada ya kuporwa
ardhi hiyo ambayo ilikuwa kama kitega uchumi chao.
No comments:
Post a Comment