Baadhi
ya wastaafu mbalimbali wakiwa tayari kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki mkoani
Pwani.Uhakiki huu unahusisha wanaolipwa kupitia Wizara ya Fedha na Mipango
Pekee.
................................................
Wizara ya Fedha na Mipango imeanza zoezi la Uhakiki wa Wastaafu
wanaolipwa na wizara hiyo katika mkoa wa Pwani, Kibaha.
Uhakiki huu hautausisha
wastaafu wanaolipwa kupitia mifuko ya hifadhi za jamii kama vile PSPF, NSSF,
PPF na GEPF.
Hayo yamebainishwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw.Mohamed Mtonga
alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari kuhusu mpango huo wa uhakiki ulioanza
leo mkoani Pwani.
“Uhakiki huu unatokana na utaratibu uliojiwekea Wizara ya Fedha na
Mipango wa kufanya uhakiki wastaafu ili kuhuisha orodha ya malipo ya wastaafu
na inasaidia kubaini mabadiliko ya taarifa za wastaafu kama vile kufariki na
hivyo kuepuka kulipa wasiostahili”Alisema Bw. Mtonga.
Aidha akizungumzia kuhusu utaratibu wa uhakiki huu amesema kuwa zoezi
hili litafanyika nchi nzima na limeanzia katika Mkoa wa Pwani wilaya ya
Kibaha na litafanyika kuanzia leo tarehe 10 mpaka tarehe 14 mwezi huu na
kuendelea kwenye wilaya zote za mkoa wa pwani mpaka tarehe 21 mwezi huu.
Baada ya uhakiki katika mkoa wa Pwani zoezi litaendeshwa kikanda nyanda
za juu kusini katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Songwe na Katavi
kuanzia tarehe 31 Octoba mpaka tarehe 11 Novemba mwaka huu.
Pia zoezi litafanyika katika kanda ya kati likijumuisha mikoa ya Dodoma,
Morogoro na Singida kuanzia tarehe 21 mpaka 25 Novemba.
Akizungumza na waandishi wa habari mwakilishi wa wazee wastaafu
Bw.Benedict Kalaguza amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kufanya uhakiki huu
wa wastaafu na kwamba zoezi limekuwa ni zuri lisilokuwa usumbufu wowote na
limeboreshwa zaidi kwa kutumia teknolojia nzuri zaidi.
Aidha Wastaafu wanaohakikiwa wanatakiwa kufika kwenye vituo hivyo wakiwa
na nyaraka kama Kadi ya Benki, Picha za passport mbili, Barua ya Ajira ya Kwanza,
Barua ya Kustaafu au kupunguzwa kazi kazini, barua ya Tuzo la Kustaafu, Nakala
ya Hati ya Malipo ya kiinua mgongo au mkupuo, kitambulisho cha pensheni na
barua ya Kudhibitishwa kazini.
No comments:
Post a Comment