Saturday, May 4, 2019

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUACHA KUSHABIKIA NDOA ZA JINSIA MOJA

 Na Ahmed Mahmoud Arusha

JESHI la polisi mkoa wa Arusha, limewataka wanahabari nchini kutokushabikia au kuunga mkono  ndoa za Jinsia moja ambazo ni vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu havikubaliki na ni kinyume cha maadili .


Rai hiyo imetolewa May 3 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana, alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari Duniani lililoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha APC kwenye ukumbi wa hotel ya Golden rose ya jijini Arusha.


Amesema kuna harakati zinazoendelea Ulimwenguni za kutaka kuungwa mkono ndoa za jinsia moja ,wanahabari wasiunge mkono vitendo hivyo na badala yake waungane pamoja kupiga vita  hata kama tutatengwa na Jumuia za kimataifa  vitendo hivyo ni kinyume cha maadili.


Amewataka wanahabari kutambua kuwa hakuna uhuru usio kuwa na mipaka hivyo akawataka wazingatia uzalendo katika kazi zao ili kuhakikisha habari zinazoandikwa zisiwe zinachafua nchi  au mkoa na Uhuru uliopo utumike  kuwalinda wanahabari wenyewe na watu wengine.


Amesema lipo tatizo  la watoto  kubakwa na kulawitiwa mkoani Arusha na wazazi huwa wanayamaliza kienyeji kwa kupitia vikao amesema anaomba wanahabari na wananchi kuwafichua watu wa aina hiyo na jeshi la polisi limewasha moto wa  kupambana na vitendo vyote vya ukatili huo.


Amewahakikishia  ulinzi wa wanahabari wanaokumbana na madhira wakati wa kutekeleza majukumu yao na kuwalinda dhidi ya vitendo vyote vya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu  ikiwemo wakati wa chaguzi za serikali za mitaa zitakazofanyika nchini kote mwaka huu.


Amewataka wanahabari kutokukubaliwa kutumiwa na watu wenye nia mbaya kuvuruga amani ya nchi na kusisitiza kuwa Arusha ni Geneva ya Afrika na anataka ibakie kuwa Geneva ya kweli kwa kutanguliza maslahi ya taifa mbele katika kutimiza majukumu yao ya kila siku .


Awali mwenyekiti wa APC,Claud Gwandu, amesema kwa siku za karibuni kumekuwepo na migogoro kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake hali ambayo inaondoa uhusiano uliokuwepo na badala yake kujenga chuki .


Amesema haoni sababu ya kugombana kati ya wanahabari na serikali na vyombo vyake,na matokeo yake ni wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola na hivyo kuibua migogoro ambayo haina ulazima.


Kauli mbiu ya mwaka huu inasema Jukumu la UTPC na Klabu za waandishi  wa habari  kuchangia uchaguzi huru na haki .

No comments:

Post a Comment