Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (
TFS) imeweka mikakati kadhaa katika kuhakikisha misitu yake inaingiza mapato ya
kutosha kupitia huduma za utalii sambamba na kuuza mazao ya misitu.
Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos
Santos Silayo amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuvitangaza vivutio vya
utalii ekolojia vilivyopo kwenye misitu ya mazingira asilia iliyo chini ya
taasisi hiyo.
Akizungumza wakati akifungua mkutano
wa nane wa baraza la wafanyakazi wa TFS lililofanyika Morogoro, Profesa Silayo
alisema aina hiyo ya utalii na biashara ya mazao ya misitu na nyuki ni nguzo ya
utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Akitolea mfano wa uvunaji wa utomvu
wa miti inayokaribia kuvunwa katika shamba la Sao Hill amesema bidhaa hiyo
inahitaji kufanyiwa utafiti na kuangalia uwezekano wa kuongeza uzalishaji wake.
Alisema katika eneo hilo pia upo
uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa gundi kutoka katika miti ya migunga, zao
linalotarajiwa kuingiza fedha nyingi siku za usoni.
Amesema ni jukumu la watumishi
kuongeza jitihada katika utendaji wao ili kuhakikisha lengo hilo hilo linatimia
na kuleta matokeo chanya.
Profesa Silayo amegusia pia suala la
udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu na nyuki pamoja na kushindwa
kuimarisha huduma katika vivutio vya utalii.
“Haya ni maeneo ambayo inabidi
tujipange vizuri zaidi kuyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili
kuondoa kero na kutoa huduma bora kwa umma.
“Endapo tutaimarisha maeneo haya,
itasaidia kuongeza tija katika jukumu letu la ukusanyaji wa maduhuli ya
Serikali, kuongeza mauzo ya nje na fedha za kigeni kupitia huduma za utalii na
uuzaji wa mazao ya nyuki,” alisema.
Pia alisisitiza kuhusu nidhamu kwa watumishi wa taasisi hiyo na kuwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake na kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi, na kusisitiza kuchukua hatua kali kwa watabainika kukiuka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Francis Kiondo alisisitiza umuhimu wa kuzungatia sheria na kanuni za utumishi wa umma kwa kila mtumishi pindi anapotekeleza majukumu yake.
No comments:
Post a Comment